Global Fund yainyima Uganda fedha

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mbunge Bahati wa Uganda aliyepeleka muswada kuhusu wapenza wa Jinsia moja

Mfuko wa Global Fund umeinyima Uganda fedha dola million 270 ilizoomba kugharimia shughuli za Ukimwi.

Hata hivyo pande mbili husika zimetofautiana kutokana sababu iliyochochea hatua hiyo.Uganda iliwahi kusifiwa duniani zamani kwa kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya Ukimwi. Mojawapo ya mbinu zikiwa ni kuwa uwazi.

Mwandishi wa BBC mjini Kampala Siraj Kalyango anasema ombi la Uganda la kupewa dola zaidi ya million 200 kuisaidia kushughulikia UKIMWI na pia kuimarisha mifumo ya kiafya kutoka Global Fund halikufanikiwa baada ya mfuko huo kukataa kutao fedha.

Meneja wa mpango wa kudhibiti UKIMWI katika wizara ya afya ya Uganda, Dr Zainab Akol,amenukuliwa na vyombo vya habari akililaumu mfuko huo kwa kukataa ombi lao la dola millioni 270 na badala yake kutoa dola millioni 130. Afisa huyo amewanyooshea kidole aliowaita wachache yaani wanaharakati wa mapenzi ya watu wa jinsia moja kwa kuifanya Uganda inyimwe fedha hizo.

Meneja huyo amesema Global Fund ilitoa maelezo kuwa sera za Uganda kuwa kali kwa wachache, yaani watu wenye mwelekeo tofauti wa masuala ya ngono.

Aidha meneja huyo amenukuliwa akisema kuwa haki za hao wachache zinapingana na mchakato wa kupiga vita dhidi ya UKIMWI na VIRUSI vyake.

Lakini Andrew Hurst anaeshughulikia masuala ya habari katika mfuko wa Global Fund ameiambia BBC kupitia barua pepe, kuwa mfuko huo ulikubali kutoa dola millioni 25 za kuimarisha mifumo ya kiafya.

Ameongeza kuwa sababu kuu ya kukataa ombi la dola 217 za UKIMWI ni fungu kubwa la pesa kutotumiwa bado kuhusu mada hiyo ilizopewa mwanzo halijatumika na kuwa na wasiwasi na uwezo wa Uganda kutumia kiasi kikubwa cha fedha kama hicho, ilhali haijamaliza fedha ilizopewa awali.

Pia amesema kuwa Uganda imeshindwa kudhihirisha matumizi sahihi hasa kwa jamii ambazo hazina uwezo. Ametaja familia zinazohitaji fedha hizo kama wale wanaotumia dawa za kulevya; watu wanofanya mapenzi ya jinsia moja, waliobadili jinsia zao, makahaba, wahamiaji pamoja na wafungwa.

Lakini matumizi ya neno wachache na meneja wa mpango wa kudhibiti UKIMWI ulikuwa katika muktadha wa watu wa mapenzi ya watu wa jinsia moja kwani ndilo linavuma nchini Uganda.

Hii ni kutokana na lawama nyingi kutoka nchi za magharibi zikiikosoa Uganda kutokana na muswaada wenye utata kuwashughulikia wapenzi wa jinsia moja ulioletwa bungeni na mbunge Bahati. Ingawa mbunge huyo anadai kuwa muswada huo una nia ya kupunguza kuenea kwa UKIMWI lakini wanaharakati wa mapenzi hayo wanadai kuwa unawalenga.

Uganda kwa sasa ina watu takriban laki saba wanaohitaji dawa za ARV, lakini ni laki tatu tu ambao wanatumia dawa hzio kwa sasa.

Hatua hii ya mfuko wa Global Fund kuinyima Uganda pesa hizo inakuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuonya mataifa kuyaonya mataifa yanayowanyanyasa wapenzi wa jinsia moja.