Kenya kutuma majeshi yake AMISOM

Jeshi la Kenya nchini Somalia Haki miliki ya picha BBC World Service

Waziri wa Mambo ya nje Moses Wetangula anaelekea mjini Rabat Morroco kunakofanyika kikao cha Jumuiya ya nchi za Kiarabu kuelezea hali ya Somalia.

Hii inafuatia mkutano kati ya Marais wa Kenya, Uganda na Somalia jana mjini Nairobi, ambapo Kenya ilitangaza kuwa tayari kushirikiana na nchi za Afrika zinazochangia askari wake katika jeshi la Umoja wa Afrika linalolinda amani nchini Somalia, AMISOM.

Wakati kampeni za kijeshi za kuwafurusha wapiganaji wa kundi la Al-Shabab kusini mwa Somalia zikipamba moto, maafisa wa kijeshi wa Kenya na serikali ya mpito wa Somalia wanaelezea kupata mafanikio makubwa dhidi ya kundi hilo katika mapigano ya hivi karibuni.

Taarifa zinasema kufuatia mapigano ya eneo la Busar katika wilaya ya El Waq mkoani Gedo , wapiganaji zaidi ya ishirini wa Al-Shabab na wengine zaidi ya thelathini kujeruhiwa.

Maafisa wa jeshi la Somalia wanasema askari wao mmoja aliuwawa na wengine watano kujeruhiwa katika mapigano hayo makali ambapo muungano wa majeshi ya Somalia na Kenya ulitumia zana mbali mnali za kijeshi zikiwemo ndege.

Al-Shabab wanaarifiwia pia kuondolewa kutoka kambi muhimu ya Talha katika eneo hilo ambapo walilazimika kuacha zana zao za kivita.

Hata hivyo kulingana na vyombo vya habari vya Somalia, maafisa wa Al-Shabab wanadai wao ndio walitekeleza mashambulizi dhidi ya majeshi ya Kenya na Somalia katika eneo hilo.

Al-Shabab pia wamedai kuwa walipata ushindi dhidi ya wanajeshi hao wa serikali y Somalia na Kenya, lakini hakuna duru zilizohuru ambazo zinathibitisha madai hayo.

Hayo yanakuja wakati waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Moses Wetangula akijiandaa kushiriki mkutano wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu mjini Rabat, Morocco kwa lengo la kuwapasha nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuhusu hali halisi ya Somalia.

Somalia ambayo imekuwa mwanachama wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu tangu mwaka wa 1974 haikupewa umuhimu mkubwa na jumuiya hiyo tangu machafuko kuzuka miaka ishirini iliyopita, isipokuwa mwaka wa 1993 ambapo baadhi ya nchi za Kiarabu zilichangia wanajeshi katika operesheni ya Restore Hope iliyo-ongozwa na jeshi la Marekani.

Miaka michache iliyopita, nchi za Kiarabu ziliahidi kuchangia wanajeshi katika operesheni ya kulinda amani Somalia, lakini ahadi hiyo hadi leo haikutimia.

Ingawa mkutano wa Rabat lengo lake kubwa ni kujadili Syria, huenda pia ukawa nafasi muhimu ya Jumuiya hiyo kuangazia upya msimamo wake kuhusu Somalia, na angalau kusaidia kifedha serikali ya Somalia, pamoja na operesheni ya kulinda amani, ambayo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha.