Askari wa Ethiopia waonekana Somalia

Mashahidi wanasema wamewaona wanajeshi mia kadha wa Ethiopia wakisafiri katikati ya Somalia.

Wazee katika eneo la Galgudud wanaripotiwa kuona msururu wa malori 14 yaliyojaa wanajeshi waliovaa sare za jeshi.

Na msafara mwengine mdogo piya ulionekana katika jimbo la jirani la Hiran.

Lakini msemaji wa wizara ya mashauri ya nchi za nje ya Ethiopia, (Dina Mufti) ameliambia shirika la habari la Ufaransa, kwamba hakuna wanajeshi wao nchini Somalia.

Ethiopia iliyaondoa rasmi majeshi yake huko Somalia mwaka wa 2009, baada ya vita dhidi ya serikali ya mahakama ya Kiislamu.

Mwezi uliopita Kenya ilituma wanajeshi wake Somalia kuwaandama wapiganaji wa kikundi cha al-Shabab.