ETIENNE TSHISEKEDI

Etienne Haki miliki ya picha
Image caption Mgombea mkongwe Tshisekedi wa Mulumba

Akiwa na umri wa miaka 79, Bw Etienne Tshisekedi, ndio mgombea mwenye umri mkubwa zaidi. Alizaliwa katika mkoa wa Kasai ya Kati mwezi Disemba mwaka 1932.

Alisomea sheria wakati wa utawala wa ukoloni wa Ubelgiji. Aliingia katika siasa wakati DRC ikipata uhuru mwaka 1960, ambapo alianza kwa kupata nyadhifa mbalimbali za ngazi ya juu serikalini, na pia katika utawala uliodumu kwa muda mfupi wa Kasai.

Alikuwa waziri wakati wa utawala wa kidikteta wa Mobutu Sese Seko, na alihamia upande wa upinzani mwaka 1980 wakati Bw Mobutu alipoamua kufuta uchaguzi wote.

Akiwa kiongozi wa chama cha UDPS, Bw Tsisekedi amekuwa mpinzani wa serikali mbalimbali tangu wakati huo.

Wakati Mobutu alipolazimishwa kuipeleka serikali yake katika mfumo wa vyama vingi mapema miaka ya 1990, Bw Tshisekedi alikuwa waziri mkuu mara mbili katika kipindi cha miaka miwili.

Aliondoka madarakani mara hizo mbili kutokana na mivutano mikali na Mobutu.

Chama cha Bw Tshisekedi hakikubeba silaha wakati wa mfululizo wa vita zilizosababisha kuanguka kwa utawala wa Mobutu mwaka 1997, na hivyo kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wananchi waliokuwa wameghubikwa na miaka mingi ya vita.

Baada ya kususia uchaguzi wa mwaka 2006, ambao alidai ulivurugwa mapema, Bw Tshisekedi ameahidi kushiriki kikamilifu safari hii na kupata ushindi.

Kwa baadhi ya watu, amevuka mipaka kwa kujitangaza kuwa ni rais kabla hata ya upigaji kura.

"Wananchi wa Kongo ni watu huru nchini humu na wamenitangaza mimi kuwa rais siku nyingi zilizopita," alisema wakati akizindua kampeni yake Novemba 11.

Wakosoaji wake wanasema matamshi kama hayo yanaweza kuchochea ghasia, hasa iwapo kama atapoteza uchaguzi.

Kukosekana kwake kwa mara kwa mara nchini humo kumeleta minon'gono kuhusu afya yake.

Bw Tshisekedi anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa katika eneo analotoka la Kasai na ia Kinshasa.

Wafuasi wake na wale wa Bw Kabila wamefarakana kwa misingi ya kikabila katika maeneo ya kusini mwa DRC, ambapo watu wengi kutoka Kasai wamehamia huko.

Chama cha UDPS kimekita mizizi yake na umaarufu upande wa kusini, lakini sio maeneo mengine nchini humo.