Iran yafanya mazoezi ya jeshi

Iran inasema kuwa imeanza mazoezi ya kijeshi ya siku nne, ili kupima uwezo wake wa kulinda mitambo yake ya nuklia na sehemu nyengine muhimu, endapo ikishambuliwa.

Shirika la habari la taifa linasema mazoezi hayo yanafanywa mashariki mwa nchi; na yanafanywa wakati mvutano umezidi baina ya Iran na mataifa makuu, kuhusu mpango wake wa nuklia, unaozusha utatanishi.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia mitambo ya nuklia, lilipitisha uamuzi Ijumaa kusema linazidi kuwa na wasiwasi kuhusu mradi wa Iran - .huku tetesi zinaongezeka kwamba Israil, huenda ikachukua hatua ya kijeshi, kuizuwia Iran kuunda silaha za nuklia.