Assad asema hajali chagizo

Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema katika mahojiano na gazeti la London la Sunday Times, kwamba anaamini kuwa msukosuko nchini mwake utaendelea, na alionesha kuitoa maanani Jumuia ya nchi za Kiarabu, ambayo imependekeza mpango wa kutafuta ufumbuzi kwa njia za amani.

Haki miliki ya picha 1

Wanaharakati wanasema makao makuu ya chama tawala cha Baath mjini Damascus, yameshambuliwa kwa makombora kadha.

Kama ripoti hizo ni kweli, basi hilo ni shambulio la mwanzo kufanywa katikati ya mji mkuu, tangu ghasia kuanza Syria mwezi wa March.

Na lilitokea punde baada ya muda uliowekwa na Jumuia ya nchi za Kiarabu kumalizika, bila ya taarifa yoyote iwapo Syria na jumuia hiyo zimefikia makubaliano juu ya mpango wa amani.

Lakini akihojiwa na gazeti la Sunday Times, Rais Assad alilalamika vikali juu ya mpango huo, akisema umekusudiwa kuonesha kuwa Waarabu wamegawanyika, na kutayarisha mambo ili mataifa ya nchi za nje yaweze kuingilia kati kijeshi; hatua ambayo itakuwa na matokeo mabaya kwa eneo zima.

Rais Assad alisema Syria haitoridhia chagizo kutoka nje, ambazo ametabiri zitaendelea.

Na serikali piya itaendelea kuzima vile alivoviita vitendo vya magaidi wenye silaha, ambao amewalaumu kwa ghasia za nchini mwake.