Idadi ya waliofariki yaongezeka Misri

Mamia ya waandamanaji nchini Misri wameivamia tena medani ya Tahrir katika mji mkuu wa Cairo hata baada ya polisi na wanajeshi kutumia nguvu kuwaondoa.

Haki miliki ya picha Reuters

Chini ya muda wa saa moja baada ya kuondolewa Tahrir,waandamanaji walirudi tena mahali hapo huku wakitoa matamshi dhidi ya utawala wa kijeshi wa Misri.

Wizara ya afya nchini humo imesema watu 22 wameuawa na takriban wengine elfu moja mia nane kujeruhiwa katika mapigano makali kati ya polisi na waandamanaji mjini Cairo.

Machafuko hayo yalianza siku mbili zilizopita.

Mamia ya wanajeshi na polisi walishambulia waandamanaji kwa risasi za raba ,gesi ya kutoa machozi na virungu.

Machafuko mengine pia yalishuhudiwa katika miji mingine ikiwemo , Alexandria, Suez na mji wa Aswan.

Wandamanaji hao ambao walikuwa wameziba nyuso zao ili gesi ya kutoa machozi isiwadhuru wanalalamika kuwa watawala wa kijeshi walikuwa na njama za kunyakuwa uongozi wa nchi hiyo.

Machafuko hayo yametokea kukiwa kumesalia wiki moja tu kabla ya uchaguzi wa maeneo bunge kuanza ambao utakuwa wa kwanza tangu Rais Hosni Mubarak kupinduliwa mwezi wa Februari.

Mwandishi wa BBC Helena Merriman amesema kuwa hali sio nzuri sana kwa sababu mara kunashuhudiwa hali ya utulivu na baadaye tena hali inabadilika na kuwa ya taharuki na watu kuanza kukimbia.

Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita makundi wa Kiiislamu pamoja na wakereketwa wengine wamekuwa wakifanya maandamano nchini Misri huku waandamanaji wakidai kuwa kuna njama za kubadilisha katiba ili kuruhusu baraza la kijeshi kuendelea kuwa na uwezo mkubwa.