Swaziland yakanusha kumfukuza Malkia Dube

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mfame Mswati wa Tatu wa Swaziland

Afisa mwandamizi wa Ufalme wa Swazi amekanusha taarifa kuwa mke wa 12 Mfalme Mswati III, Nothando Dube, amefukuzwa katika kasri la Kifalme.

Malkia Dube ameliambia gazeti la Afrika Kusini la kila Jumapili Sunday Times kuwa aliamriwa ‘kufungasha vitu vyake na kuondoka’ zaidi ya wiki moja iliyopita baada ya kumnyunyizia mlinzi maji ya pilipili.

Lakini gavana katika ofisi ya Kifalme Timothy Velabo Mtetwa ameliambia gazeti la Times of Swaziland amekwenda kumtembelea bibi yake.

Mwaka uliopita, Malkia Dube, mwenye umri wa miaka 23, alikanusha tuhuma za kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje.

Katika mahojiano na gazeti binafsi Malkia Dude alisema amekuwa na mabishano na mlinzi aliyekataa kumruhusu kutoka nje ya kasri Jumamosi iliyopita.

Alitaka kumpeleka mtoto wake mdogo kati ya watatu mwenye umri wa miaka miwili hospitali baada ya kujiumiza wakati akicheza, lakini mlinzi hakumruhusu kuondoka, taarifa zinasema.

Tuhuma zilizotolewa na gazeti la Afrika Kusini hazina msingi wowote kwani Malkia Dude aliondoka na walinzi wake.”Timothy Velabo Mtetwa Gavana wa Kifalme alisema.

Malkia huyo alisema matokeo ya mzozo huo ni kuwa alizuiwa kwa nguvu kuondoka kwenye kasri.

"Sikuwa na budi ila kujilinda mwenyewe hivyo nikamnyunyizia pilipili kwenye macho," Malkia Dube aliliambia Sunday Times.

Kisa hicho kikaripotiwa kwa Malkia Kiongozi ambaye moja kwa moja aliamua kuwa Malkia Dube amekosa heshma na alitakiwa kufukuzwa.

"Sikuweza hata kuchukua vitu vyangu vyote, kwa sababu walisema tu 'fungasha vitu vyako na uondoke sasa hivi’," alinukuliwa akisema.

Aliwaacha watoto wake kwenye kasri.

Lakini Bw Mtetwa ameliambia gazeti binafsi la Times of Swaziland, ‘Si kweli kabisa’ kuwa Malkia Dude amefukuzwa.

Gavana huyo amesema kiutamaduni mtu anapofukuzwa kwenye himaya ya Kifalme watu wawili wanatakiwa kubeba vitu vyake nje lakini katika tukio hili Malkia Dude aliondoka kwa amani kumtembelea bibi yake, taarifa zinasema.

"Tuhuma za gazeti la Afrika Kusini hazina ukweli wowote kwa sababu Malkia Dude aliondoka na walinzi wake ambao kwa sasa wanamlinda kwa tahadhari kwa kuwa bado ni sehemu ya familia ya kifalme," gazeti limemnukuu akisema.

Mwezi Agosti, Waziri wa Sheria wa Swaziland Ndumiso Mamba alijiuzulu kufuatia tuhuma kuwa alikuwa na mahusiano na malkia Dube,ambaye ameripotiwa kuwa chini ya ulinzi tangu wakati huo.

Amekanusha tuhuma hizo.

Mfalme Mswati ambaye ni pekee aliyebakia mwenye mamlaka kamili kwa sasa yuko mapumziko ya mwaka kama sehemu ya kujitakasa kiorho.

Anatarajiwa kurejea mwezi Januari.