Serikali ya Burundi yadaiwa kuua waasi

Image caption Burundi: Mauaji yanadaiwa kutekelezwa na chama tawala na makachero

Kikundi cha kutetea haki za binadamu kimedai kuwa watu mia tatu waliokuwa wanachama wa kundi moja la waasi, la National Liberation Front- FNL wameuawa.

Inadaiwa mauaji haya yametekelezwa na wafuasi wa chama tawala au makachero.

Shirika la Haki za Binadamu, na Shirika lingine la kufuatilia vitendo vya serikali, wamesema mauaji hayo yalifanyika miezi mitano iliyopita.

Katika tukio lingine, watu kumi na wanane wanaodhaniwa kuwa wahalifu wa kutumia silaha wameuawa mashariki mwa nchi hiyo.

Burundi inarejea katika hali ya amani baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka 2009 wakati waasi wa FNL walipoweka chini silaha baada ya miongo miwili ya mgogoro nchini humo.