Makabiliano yaendelea karibu na Tahrir

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Makabiliano katika medani ya Tahrir mjini Cairo

Bado kuna hali ya wasiwasi mjini Cairo huku waandamanaji wakiongeza kasi katika harakati zao za kutaka watawala wa kijeshi wajiuzulu.

Kumekuwa na makabiliano katika barabara za mji huo huku idadi ya polisi wa kuzuia fujo ikiongezeka hasa katika jengo la wizara ya mambo ya ndani lililoko karibu na medani ya Tahrir.

Waandamanaji wamekataa ahadi ya baraza la kijeshi linalotawala kuharakisha mabadiliko ya kupatikana kwa serikali ya kiraia.

Mwandishi wa BBC Jeremy Bowen mjini Cairo anasema kuwa machafuko hayo yanatishia uchaguzi wa wabunge unaotarajiwa wiki ijayo.

Anasema maoni ya watu juu ya maandamano hayo yamegawanyika. Baadhi ya raia wa Misri wanataka uchaguzi huo ufanyike bila usumbufu wowote huku wengine wakiamini kuwa lazima jeshi liondolewe madarakani kwanza.

Baraza la kijeshi limepewa jukumu la kuongoza nchi katika mabadiliko hadi kuwe na demokrasia.Maandamano ya hivi karibuni yamechochewa na wasiwasi kuwa jeshi lina nia ya kuendelea kubaki madarakani.

Siku ya Jumanne mkuu wa Baraza la kijeshi Mohamed Hussein Tantawi, alijaribu kutuliza hali hiyo kwa kuahidi uchaguzi wa urais kufikia mwishoni mwa mwezi Juni mwaka ujao. Baraza la mawaziri la kiraia liloteuliwa na jeshi pia lilijiuzulu.