Jeshi Misri 'lamteua Waziri Mkuu' mpya

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kamal Ganzouri akubali kuunda serikali mpya

Watawala wa kijeshi nchini Misri wamemteua waziri mkuu wa zamani Kamal Ganzouri aweze kuunda serikali mpya, shirika la habari la serikali limesema.

Baraza la mawaziri la kiraia lilokuwa limeteuliwa na jeshi lilijiuzulu mapema wiki hii wakati maandamano yalipoanza mjini Cairo na miji mingine.

Baraza la kijeshi limesema kwa uchaguzi wa wabunge utaanza wiki ijayo kote nchini kama ilivyopangwa.

Makabiliano karibu na medani ya Tahrir yamepungua lakini wanaharakati wanakataka kuwe na maandamanano siku ya Ijumaa.

Idadi kubwa ya waandamanaji wanalala katika medani ya Tahrir wakijiandaa kwa mkutano mkubwa siku ya Ijumaa.

Baraza kuu linalotawala la kijeshi linasimamia mchakato wa mabadiliko hadsi katika utawala wa kiraia kufuatia kupinduliwa kwa Rais Hosni Mubarak mwezi Februari.

Licha ya ahadi za baraza hilo kuharakisha mchakato wa mabadiliko, raia wengi wa Misri wanaogopa kuwa jeshi lina nia ya kuendelea kubaki madarakani.

Bwana Ganzouri aliongoza serikali ya Misri kutoka mwaka 1996 hadi mwaka 1999 chini ya utawala wa Bwana Mubarak.

Gazeti la serikali al-Ahram limesema katika tovuti yake kwamba kimsingi Bwana Ganzouri amekubali kuongoza serikali baada ya kukutana na kiongozi wa baraza la kijeshi Mohamed Hussein Tantawi.

Bwana Ganzouri, ambaye amejitenga na utawala wa Bwana Mubarak, amependekezwa kama mgombea wa urais.