Mihadhara ya kampeni imefutwa Congo

Polisi katika Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, wamepiga marufuku mikutano ya hadhara kwa sababu ya mvutano kuzuka baina ya pande zinazoshindana, siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu nchini humo.

Haki miliki ya picha

Mkuu wa polisi, Jean de Dieu Oleko, alisema mikutano yote imefutwa.

Rais Joseph Kabila na wapinzani wake wawili wakuu, wakitarajiwa kufanya mikutano ya hadhara leo karibu-karibu.

Mwandishi wa habari wa Reuters anaarifu kuwa aliona watu wakirushiana mawe, na afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, alimwambia kuwa mtu mmoja ameuwawa.

Mwandishi wa BBC mjini Kinshasa anasema, gavana wa jiji piya aliwaambia waandishi wa habari, kwamba mihadhara imevunjwa, kwa kuhofia kunaweza kutokea mapambano kati ya wafuasi.

Mikutano ya wagombea wakuu wa urais ilipangwa kufanywa kwenye mitaa inayokaribiana.

Wafuasi walianza kuzozana tangu uwanja wa ndege, ambako walikwenda kuwapokea viongozi wao waliokuwa wakirudi baada ya kufanya kampeni mikoani.

Wafuasi walirushiana mawe na kuwarushia polisi piya.

Mwandishi wetu anasema inatarajiwa kuwa uchaguzi utafanywa Jumatatu kama ilivopangwa.