Mashirika yasikitishwa na ghasia Congo

Mashirika ya kimataifa, pamoja na Umoja wa Mataifa yamesema yanasikitishwa na ghasia zilizotokea jana katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, ambapo watu wane walikufa.

Haki miliki ya picha Associated Press

Kiongozi mmoja wa upinzani anasema waliokufa ni zaidi.

Na mpinzani mkuu, Bwana Etienne Tshisekedi, ametaka kukaidi amri ya kutofanya kampeni leo, mkesha wa uchaguzi, na alipanga kufanya mkutano wa hadhara.

Lakini taarifa zinasema polisi wameingilia kati kuzuwia mkusanyiko huo.

Bwana Tishisekedi anadai kuwa alinyimwa kufanya mkutano jana, pale polisi walipoingilia kati wakati mapambano yalipozuka baina ya wafuasi tofauti, na wafuasi na polisi.

Msemaji wa maswala ya siasa wa Bwana Tshisekedi, Valentine Mubaki alisema wao hawatovunja sheria kwa kufanya mkutano leo, kwa sababu sheria ilivunjwa jana:

"Kwanini Kabila anasema hatuwezi kufanya mkutano leo.

Sheria aliivunja yeye jana kwa kumkamata mgombea mwenzake na kumzuwia asifanye kampeni.

Alivunja sheria.

Alitoka katika sheria.

Sasa hawezi kurejea tena kutaka kutekeleza sheria, kwa kutukataza kufanya mkutano leo, wakati sheria amekwishazivunja"

Huku nyuma, tume ya uchaguzi imesema uchaguzi utafanywa kesho kama ilivopangwa.