Uchaguzi wa Misri waingia siku ya pili

Maafisa wa usalama wakilinda wapigaji kura Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maafisa wa usalama wakilinda wapigaji kura

Raia wa Misri walijitokeza kwa wingi kupiga kura ya kuwachagua wabunge siku ya Jumatatu, ukiwa ni uchaguzi wa kwanza kufanyika tangu kung'olewa madarakani kwa Rais Hosni Mubarak, mwezi Februari.

Vituo vya kupigia kura vilifungwa baada ya baraza la kijeshi linalotawala nchini Misri kuongeza muda wa saa mbili, wakati wa upigaji kura.

Muda wa kupiga kura uliongezwa ili kuwawezesha watu waliokuwa kwenye foleni kupata fursa ya kupiga kura.

Kulikuwa na taarifa za upungufu wa karatasi za kupigia kura, masanduku ya wino, wakati ambapo baadhi ya majaji waliokuwa wakifuatilia uchaguzi huo walipotea njia walipokuwa wakielekea kwenye vituo vya kupigia kura.

majeruhi

Zaidi ya watu 25 walijeruhiwa katika matukio kadha ya mapigano. Lakini waangalizi hawajatoa taarifa yoyote ya kuwepo matukio ya kutisha au ukiukaji wa taratibu za uchaguzi.

Upigaji kura unaendelea leo.

Siku ya kwanza ya upingazi kura ilikuwa tulivu, japo waandamanaji katika medani ya Tahrir walisusia uchaguzi huo wa wabunge.

Takriban watu millioni 50 wamejiandikisha kupiga kura katika nchi yenye zaidi ya watu millioni 85.