Wanawake wabakaji Zimbabwe mahakamani

Mipira ya Kondomu
Image caption Mipira ya Kondomu

Polisi wa Zimbabwe wanaamini kuna mtindo wa wanawake kuwabaka wanaume Zimbabwe , ili kutumia mbegu zao za kiume katika ushirikina kujitajirisha.

Imechukuwa zaidi ya mwaka mmoja polisi kuwakamata wahusika na siku ya Jumatatu wanawake watatu walifikishwa mbele ya mahakama katika mji mkuu Harare kwa mashtaka ambayo yameishangaza nchi nzima.

Mtu mmoja aliyepitia madhila hayo hakutaka jina lake kutajwa, alielezea yaliomkuta katika televisheni ya taifa mwezi July ambapo tukio hilo lilitokea baada ya yeye kupewa lifti na kundi la wanawake watatu mjini Harare. "Mmoja wa wanawake hao alinurushia maji usoni na baadae wakanidunga sindano iliyonipa uchu wa kutaka kufanya ngono" alisema bwana huyo.

"Waliisimamisha gari na kunilazimisha kufanya tendo la ngono na kila mmoja wao nikitumia mipira ya Kondomu.Baada ya kumaliza shughuli hiyo waliniacha mwituni uchi wa mnyamaa".

"Watu waliokuwa wakikata nyasi walinisaidia kuwaita Polisi, walionipeleka hospitali kupata matibabu kutokana na ile dawa niliyodungwa kwa kuwa bado nilikuwa na hamu isiyopungua ya kufanya ngono" Aliongeza mwanamume huyo

Wanawake hao wanatarajiwa mahakamani kwa mashtaka 17 ya kumdhalilisha na kumlazimisha mtu kufanya asilolitaka-sheria nchini Zimbabwe haitabui ama haina kipengee kuhusu kitendo cha mwanamke kumbaka mwanamume.

Wanawake hao walizuiliwa mapema mwaka huu katika mji wa kati wa Gweru, 275km (maili 170) kusini-magharibi mwa Harare, baada ya maafisa kugundua mipira 31 ya kondomu iliyotumika, katika gari waliokuwa wakisafiria. Wanawake hao wamekanusha mashtaka wakisema kuwa wao ni makahaba na walikuwa na shughuli nyingi zilizowanyima fursa ya kutupa mipira hiyo ya Kondomu.