Djibouti yajiunga na AMISOM Somalia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption AMISOM Somalia

Majeshi ya Djibouti yamewasili kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kuunga mkono jeshi la askari 9,000 wa umoja wa Afrika AU wanaopambana na wapiganaji wa al-Shabab.

Ni nchi ya tatu tu kujiunga na jeshi la AU, linalosema linahitaji majeshi ya ziada kudhibiti maeneo yanayoshikiliwa na al-Shabab.

Kenya pia imesema majeshi yake yaliyopo Somalia ya kusini yatungana na majeshi ya AU.

Al-Shabab lenye uhusiano na al-Qaeda linapigana kuondosha serikali ya mpito ya Somalia inayoungwa mkono na umoja wa mataifa.

Kundi hilo linakadiriwa kuwa na wapiganaji 7,000 hadi 9,000 na kudhibiti maeneo mengi ya kati na kusini mwa nchi hiyo.

Mwezi Agosti, lilitangaza kujiondoa Mogadishu baada ya mapigano makali na majeshi ya AU.

Ahadi zilizovunjwa

Lakini kundi hilo limeendelea kulipua mabomu mjini humo, na kuua watu watano katika shambulio lililofanyika eneo lenye watu wengi mapema mwezi huu.

Makamanda wa AU walisema wanahitaji hadi majeshi 20,000 kudhibiti mji wa Mogadishu.

Mwandishi wa BBC Mohamed Dore mjini Mogadishu alisema ndege iliyokuwa imebeba majeshi ya Djibouti imetua mjini humo.

Inaaminiwa kuwa majeshi hayo ni zaidi ya 800 na kuongeza nguvu majeshi ya AU, ambayo kwa sasa inajumuisha majeshi ya Uganda na Burundi.

Nchi nyingine zilizoshindwa kutimiza ahadi zao za kutuma majeshi ni Nigeria na Malawi.

Djibouti iko mpakani mwa Somalia na watu wake wanazungumza lugha moja.

Kenya ilituma majeshi yake mwezi Oktoba kupambana na al-Shabab baada ya kuwalaumu wapiganaji hao kufanya utekaji nyara katika mpaka wa nchi hiyo.

Wapiganaji hao wamekana kuhusika katika utekaji nyara huo.

Somalia haijawa na serikali thabiti kwa zaidi ya miaka 20 na imejikuta kwenye mapigano kutoka makundi mbalimbali ya wapiganaji.