Kabila aongoza kwenye uchaguzi DRC

Image caption Bw Joseph Kabila

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anaongoza kwa asilimia 46 ya kura zote, matokeo yanavyoonyesha.

Ikiwa zaidi ya robo tatu ya kura zikiwa zishahesabiwa, mpinzani wake mkuu, Etienne Tshisekedi, ana aslimia 36, tume ya uchaguzi imesema.

Malori yaliyobeba polisi wa kuzuia ghasia wanapiga doria katika miji mikuu iwapo patatatokea vurugu, matokeo yote yakitarajiwa kutolewa siku ya Jumanne, huku kukiwa na madai ya kuwepo udanganyifu.

Takriban watu 3,000 walikimbia mji mkuu, Kinshasa, mwishoni mwa juma.

Uchaguzi wa Jumatatu iliyopita ni wa pili kufanyika tangu vita vya mwaka 1998-2003 kumalizika rasmi, ambapo takriban watu milioni nne walifariki dunia.

Makundi yenye silaha yanaendelea kufanya shughuli zao mashariki mwa nchi hiyo, yenye ukubwa wa theluthi mbili ya Ulaya ya Magharibi.

Mwandishi wa BBC Thomas Fessy mjini Kinshasa alisema wafuasi wa Bw Tshisekedi wanasisistiza kashinda na kuna uwezekano mkubwa hawatokubali kushindwa katika uchaguzi uliogubikwa na madai ya wizi wa kura.

Wakongo wapinga nje ya nchi

Haki miliki ya picha VT Freeze Frame
Image caption Bw Etienne Tshisekedi

Hata hivyo, mkuu wa tume ya uchaguzi alisema siku ya mwisho iliyowekwa ya Jumanne kutangaza matokeo yote huenda isifikiwe.

Daniel Ngoy Mulunda, alisema, "Kwanza tutahakikisha makaratasi yote ya matokeo yamefika na tuna taarifa zote. Kama sivyo, hatutoweza kuwapa zaidi ya matokeo machache tu."

Afisa mwandamizi aliye karibu na Bw Kabila ameonya kuwa jeshi linaweza kusambazwa iwapo "hali itakuwa na vurugu sana ya kuwazidi polisi".

"Hatuwezi kuacha ghasia ziendelee," Kikaya Bin Karubi, balozi wa Kongo nchini Uingereza amenukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Polisi walirusha mabomu ya machozi kwa wafuasi wa upinzani kwenye mji mkuu siku ya Jumatatu, na milio ya risasi ilisikika kwenye jimbo la Kasai Magharibi, maeneo yote yakiwa ngome za upinzani, baada ya serikali kufunga kituo cha televisheni na redio, shirika la Reuters lilisema.

Kulikua na ghasia zaidi Jumatatu usiku nje ya nyumba ya Bw Tshisekedi mjini Kinshasa na kwenye makao makuu ya chama chake cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), mwandishi wetu alisema.

Wanaomwuunga mkono Bw Tshisekedi walifanya maandamano Afrika Kusini, na Ubelgiji, nchi iliyokuwa koloni lake, siku ya Jumatatu wakitaka atanagzwe kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Waanadamanji hao walijaribu kuuvamia ubalozi wa Kongo mjini Pretoria, na kuwalazimu polisi kurusha mabomu ya kutoa machozi, shirika la AFP limeripoti.

Waandamanaji wamemshutumu rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kwa kusaidia kuandaa uchaguzi uliojaa udanganyifu huko Kongo na kutaka asijihusishe na masuala ya nchi hiyo.