Mgambia atarajiwa kumrithi Ocampo ICC?

Haki miliki ya picha
Image caption Fatou Bensouda

Fatou Bensouda anatarajiwa kutajwa kuwa mwendesha mashtaka mkuu mpya wa mahakama ya kimataifa ya ICC.

Wakili huyo mwenye umri wa miaka 50 kutoka Gambia ni naibu wa Luis Moreno-Ocampo, ambaye muda wake unaisha mwakani.

Awali alifanya kazi kama mwanasheria katika mahakama ya kimataifa ya Rwanda nchini Tanzania.

Kesi zote za ICC mpaka sasa zinatoka Afrika, na baadhi ya viongozi wa bara hilo wameilaumu mahakama hiyo kwa kuwatia hatiani Waafrika tu.

Mrithi wa Luis Moreno-Ocampo atachaguliwa rasmi na baraza kuu la mataifa yaliyoridhia mahakama hiyo- chombo kinachowakilisha nchi 119 zinazoiunga mkono mahakama hiyo- katika mkutano wao wa mjini New York Desemba 12.

Hata hivyo, rais wa ASP, Balozi wa Umoja wa Mataifa wa Liechtenstein Christian Wenaweser, amesema kwa sasa Bi Bensouda ndiye mgombea pekee.

Ilikubalika kuwa mrithi wa Bw Ocampo lazima awe Muafrika na inaarifiwa mgombea pekee, Mohamed Chande Othman wa Tanzania, alijitoa.

Bw Wenaweser aliliambia shirika la habari la Reuters kwa simu, " Nitapendekeza katika mkutano wa Desemba 12, kwa kuzingatia ushauri, tusonge mbele na mgombea mmoja Fatou Bensouda."

ICC, yenye makao makuu yake The Hague, ni mahakama ya kwanza ya kudumu duniani ya uhalifu wa kivita iliyoanza shughuli zake 2002.

Fatou Bensouda aliliambia shirika la AFP yeye alikuwa akiwafanyia kazi waathirika wa Afrika.