Haki za watu wa jinsia moja zashinikizwa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bi Hillary Clinton

Marekani imetangaza hadharani kuwa itapambana na ubaguzi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja nchi za nje kwa kutumia msaada kutoka nchi za kigeni na diplomasia kushinikiza mabadiliko.

Waziri wa mambo ya nje Hillary Clinton aliwaambia wanadiplomasia Geneva: "Haki za wapenzi wa jinsia moja ni haki za binadamu".

Taarifa kutoka utawala wa Obama inayaelekeza mashirika ya serikali ya nchi hiyo kuangazia haki za wapenzi hao wanapofanya uamuzi wa kutoa misaada na uhifadhi wa kisiasa.

Sera kama hizo tayari zinatumika kwa usawa wa kijinsia na ghasia za kikabila.

"Isiwe jambo la uhalifu kwa mtu kufanya mapenzi ya jinsia moja," Bi Clinton alisema katika umoja wa mataifa Geneva, akiongeza kuwa utamaduni au dini siyo sababu ya kufanya ubaguzi.

Wanadiplomasia hao pia ilihusisha wawakilishi kutoka nchi ambazo mapenzi ya jinsia moja ni uhalifu.

Mabalozi wengi waliondoka kwenye ukumbi huo mara tu baada ya Bi Clinton kumazlia hotuba yake, shirika la habari la AP liliripoti.

Mwezi Oktoba, pendekezo la waziri mkuu wa Uingereza David Cameron la kupunguza misaada kwa nchi zisizotambua haki za wapenzi wa jinsia moja lililaaniwa na nchi nyingi za Afrika ambapo vitendo hivyo vimepigwa marufuku, zikiwemo Ghana, Uganda na Zimbabwe.

Wiki iliyopita Nigeria ilikuwa nchi ya barani Afrika ya hivi karibuni iliyokuwa ikijaribu kuongeza nguvu katika sheria za wapenzi wa jinsia moja, huko bunge la senate likipitisha muswada wa kupiga marufuku ndoa za watu wa jinsia moja.

Kabla haijawa sheria lazima ipitishwe na bunge dogo, baraza la wawakilishi, na kisha kutiwa saini na Rais.