Nigeria yawakamata Boko Haram

Mmoja wa kiongozi wa wapiganaji wa kundi la kiislamu la Nigeria Boko Haram amekamatwa baada ya kufyatuliana risasi kwenye mji wa Kano.

Muhammed "Hamza" Aliyu alikamatwa wakati akijaribu kuondoka mjini hapo baada ya watu saba kuuawa katika mapambano hayo ya risasi nje ya nyumba yake, polisi walisema.

Hata hivyo, chanzo kilicho karibu na Boko Haram kimekataa kwamba Bw Aliyu ni miongoni mwa kiongozi wa kundi hilo.

Boko Haram limefanya mashambulio kadhaa kaskazini mwa Nigeria na ya kati.

Kundi hilo, ambalo jina lake linamaanisha kupiga marufuku elimu ya kimagharibi, aghlabu hulenga majeshi ya usalama na taasisi za taifa.

Mwezi Agosti kundi hilo lilidai kuhusika na shambulio la bomu kwenye makao makuu ya umoja wa mataifa nchini Nigeria, katika mji mkuu wa Abuja, lililosababisha vifo vya takriban watu 23.

Mwandishi wa BBC Abdullahi Kaura Abubakar alisema mpaka wiki iliyopita, Kano, mji mkubwa kabisa kaskazini mwa Nigeria, umenusurika kwenye mashambulio ya hivi karibuni ya ghasia.

Siku ya Alhamis usiku, wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi hilo walishambulia shule ya sekondari karibu na mji huo, na kuua maafisa wa anga wanne, vyanzo vya hospitali vilisema.

Jumamosi, Bw Aliyu alishuku kuwa nyumba yake inachunguzwa na kuwaita wanachama wa kundi hilo kuwashambulia polisi iliyosababisha ufyatulianaji huo wa risasi, alisema mkuu wa polisi wa jimbo la Kano Ibrahim Idris.

Alisema maafisa watatu wa polisi na wanamgambo wanne waliuawa.

Silaha na risasi zilizoshukiwa kuibiwa kwenye mashambulio ya hivi karibuni katika vituo vya polisi Nigeria ya kaskazini zilikutwa kwenye gari lake, huku vifaa vya kutengenezea mabomu vilikutwa nyumbani kwake, mkuu huyo wa polisi alisema.

Bw Idris alisema watu 14 walitiwa kizuizini.