Shambulio la Kenya laua raia Somalia

Haki miliki ya picha 1

Takriban raia 15 wameuawa katika mashambulio mawili ya anga katika kijiji kinachodhibitiwa na wapiganaji wa kiislamu nchini Somalia karibu na mpaka wa Kenya, walioshuhudia wameiambia BBC.

Jeshi la Kenya limethibitisha kufanya mashambulio mawili ya anga katika kambi ya al-Shabab eneo la kijiji cha Hosingow, na kuua wanamgambo 17.

Mashambulio ya guruneti ya hivi karibuni kwenye mpaka karibu na kambi ya wakimbizi ya Dadaab yalipangwa kutokea Hosingow, jeshi la Kenya limesema.

Kenya ilipeleka majeshi Somalia mwezi Oktoba kwa minajil ya kupambana na al-Shabab.

Iliishutumu kundi hilo lenye uhusiano na al-Qaeda, linalodhibiti eneo kubwa la Somalia ya kati na kusini, kwa kufanya utekaji nyara kwenye eneo lao- madai ambayo wanamgambo hao wameyakataa.

Al-Shabab limesema wanaona kuwepo kwa majeshi kusini mwa Somalia kama nia ya kutaka vita.

Mashambulio hayo yamefanyika siku ya Jumanne, msemaji wa jeshi la Kenya Meja Emmanuel Chirchir alisema kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter.

Kamanda mwandamizi wa al-Shabab, afisa utawala wa al-Shabab na wapiganaji 15 walikufa kwenye mashambulio hayo mawili, aliiambia BBC.

Alisema, "hakuna raia wowote waliojeruhiwa kwenye mashambulio hayo."

Lakini mmoja aliyeshuhudia huko Hosingow, Abdallahi Abdi Mahad, aliiambia idhaa ya Kisomali ya BBC kuwa raia 15 walifariki dunia, ikiwemo familia nzima kwenye nyumba moja, na zaidi ya watu 20 walijeruhiwa.

Alisema, ukizingatia ukosefu wa hospitali eneo hilo, kuna uwezekano wa kuwepo vifo na majeruhi zaidi.

Alisema shambulio la kwanza lilifanyika nje ya kijiji hicho na la pili limepiga moja kwa moja kwenye kijiji hicho.

Mwengine aliyeshuhudia, Ahmed Yusuf, aliliambia shirika la habari la AFP, "bomu moja lilirushwa karibu na mtaa ambapo watu walikuwa wakifanya biashara zao."