Maafa 'Uvamizi wa mifugo' Sudan Kusini

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mifugo Sudan

Shambulio lililofanywa Sudan kusini katika kijiji kimoja limesababisha mauaji ya watu takriban 41, kulingana na taarifa za serikali.

Tukio hilo limetokea katika jimbo la Jonglei, lililo maarufu sana kwa mapigano ya kikabila na wizi wa mifugo.

Sudan kusini imepata tu uhuru wake mwezi Juali, lakini ukosefu wa usalama ni moja ya changamoto kubwa inayoikumba nchi hiyo.

Kijiji cha Jalle kilishambuliwa kwa risasi kutoka kwa msururu wa watu waliokuwa na silaha. Wengi wa waliouawa ni wanawake na watoto.

Mtoto mmoja mchanga aliuawa kwa upanga kwa mujibu wa gavana wa Jimbo la Jongley, Kuol Manyang aliyezungumza na BBC.

Wengine waliuawa kwa kuchomwa moto wakiwa hai walipojaribu kujificha ndani ya nyumba zao za nyasi.

Walionusurika na kutoroka walililaumu kundi la kabila la Murle, na pia alisema baada ya mauaji hayo waliondoka na mifugo.

Akitoa tathmini ya tukio hilo, gavana alisema wavamizi hao huenda walitembea kwa muda wa siku nne kutoka kwao ili kufanya shambulio hilo.

Aliongeza kuwa baadhi ya wale walioponyoka mauaji hayo walijaribu kuwafuata washambuliaji, jambo ambalo bila shaka litasababisha mapigano zaidi.

Umiliki wa mifugo ni sehemu ya utamaduni kama utajiri kwa watu wengi wa makabila ya Sudan kusini.

Wizi wa mifugo imekuwa tabia na maisha kwa wengine. Ni vigumu kukomesha tabia ya aina hiyo katika Sudan kusini.

Barabara kwa kawaida hazipitiki, na hivyo kuwafanya askari wa usalama kushindwa kupita kutekeleza kazi yao.

Vita vya miaka mingi vinamaanisha kuwa raia wengi wanamiliki silaha. Na kulipiza kisasi wizi wa mifugo ni jambo linalorudiwa sana.

Mwezi Agosti zaidi ya watu 600 waliuawa ndani ya siku moja katika jimbo la Jonglei.

Wakuu wanasema tume ya kuhifadhi amani ya Umoja wa Mataifa pamoja na kanisa yanajaribu kushawishi pande zote zijitahidi kuhifadhi amani.

Lakini kila mmoja anafahamu hali ya usalama ya Jonglei, ni mbovu na unaisababishia serikali changamoto kuliko mengine yote.