TI: Vurugu zinatokana na ufisadi

Ripoti kuhusu ufisadi ya Transparency International
Image caption Ripoti kuhusu ufisadi ya Transparency International

Shirika la kupambana na ufisadi, Transparency International,limesema ghasia ambazo zimeshuhudiwa kote duniani kwa kiwango fulani zimetokana na ufisadi.

Katika uchunguzi wake kwa nchi 183 unaotolewa kila mwaka, Transparency International imesema nchi ambazo zimeshuhudia vurugu hizo ndizo ambazo zimefanya vibaya katika kukabiliana na ufisadi.

Mwaka huu shirika hilo limegundua kuwa nchi zilizohusika na mapinduzi katika mataifa ya kiarabu kama vile Misri, Algeria, Libya na Syria zikiwa chini katika orodha hiyo ya mataifa yaliyo na ufisadi mkubwa zaidi.

Uchuguzi wake aidha unaonyesha nchi nyingi zinazotumia sarafu ya Euro ambazo zinakabiliwa na wakati mgumu kiuchumi pia zinafanya vibaya katika kukabiliana na ufisadi.

rushwa na kodi

Uchunguzi huo unasema kushindwa kwa maafisa wa umma kukabiliana na rushwa na watu wanaokwepa kulipa kodi, ndio sababu kuu zinazochochea mzozo wa madeni katika mataifa hayo.

Katika ripoti hiyo ya Transparency International nchi ya New Zealand imeorodheshwa ya kwanza kama nchi isiyokuwa na visa vingi vya ufisadi.

mataifa bora Afrika

Barani Afrika, Botswana inaongoza ikiwa nambari 39, kama nchi isiyokuwa na ufisadi wakati Somalia imeibuika ya mwisho kama nchi ambako ufisadi unashuhudiwa kwa kiwango kikubwa.

Rwanda imepongezwa kwa kupiga hatua katika kukabiliana na ufisadi.

Shirika la Transparency International linamalizia kwa kusema '' serikali fisadi ni serikali ambayo iko katika hatari ya kuangamia''.