Sudan yasitisha kumtimua Balozi wa Kenya

Omar al-Basir Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Sudan Omar al-Bashir asitisha uamuzi wa kumtimua balozi wa Keny, Sudan

Rais wa Sudan Omar al Bashir amebatilisha uamuzi wa kumtimua balozi wa Kenya nchini Sudan baada ya kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Kenya Moses Wetangula na waziri wa ulinzi Yusuf haji.

Mkutano kati ya viongozi hao ulifanyika mjini Khartoum katika juhudi za kutatua mzozo wa kidiplomasia kati ya Kenya na Sudan.

Mzozo huo uliibuka baada ya mahakama kuu nchini Kenya kutoa amri ya kukamatwa kwa Rais wa Sudan iwapo ataingia nchini Kenya.

Rais Bashir anatakiwa na mahakama ya ICC kutokana na tuhuma za mauaji ya halaiki katika eneo la Darfur.

Waziri Wetangula ameiambia BBC kuwa rais Bashir ameondoa vikwazo vyote alivyokuwa ameweka dhidi ya Kenya.

‘Alikuwa ameamua kumfukuza balozi wa Kenya, kufunga anga ya Sudan kwa ndege zinazokuja kutoka Kenya, kufukuza askari wa Kenya wanafanya doria kule Darfur, katika kikosi cha Umoja wa Mataifa...'

Kwa mujibu wa Wetangula Rais Bashir alikataa kutoshiriki katika vikao vinavyoongozwa na Kenya kama mwenyekiti wa IGAD kuhusu mambo ya CPA, na mambo mengine ya biashara ambayo Sudan ni namba tano kwa ununuzi wa chai kutoka Kenya.

Balozi wa Kenya, Robert Mutua Ngesu, alitimuliwa Novemba 29 siku moja baada ya mahakama Kuu mjini Nairobi ilitoa uamuzi wa kutaka serikali kumkamata na kumkabidhi Al-Bashir kwa ICC iwapo atakanyaga ardhi ya Kenya tena.

Sudan pia ilimtaka balozi wake kutoka Kenya lakini Nairobi imemtaka balozi huyo asiondoke.

Waziri Wetang'ula ameshutumu uamuzi huo wa mahakama akiuita "hukumu yenye makosa " na ambayo imeshindwa kutafakari uwiano wa uhusiano wa kimataifa.

Amri hiyo iliendana na ziara ya Rais Al-Bashir aliyofanya Kenya tarehe 27 Agost 2010, siku ambayo Kenya ilizindua katiba yake mpya.