Mzozo wa Euro waitishia Afrika

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Baadhi ya sarafu za euro zikionekana kuwaka moto, mzozo wake watishia barala Afrika

Mawaziri wa fedha katika nchi mbili zinazoongoza kiuchumi barani Afrika wameishutumu Jumuiya ya Ulaya kwa kushindwa kudhibiti kuenea kwa mzozo wa madeni unaoukabili ukanda wa sarafu ya Euro

Kwenye mahojiano na BBC, Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini Pravin Gordhan na mwenzake wa Nigeria Ngozi Okonjo-Iweala, wote wawili wamesema kuyumba kwa thamani ya sarafu ya Euro na kupanda kwa bei za bidhaa kunatishia matumaini ya ukuaji wa uchumi barani Afrika.

Ingawa sio mara ya kwanza kwa Bwana Gordhan kuzungumzia kuhusu athari za sera za kiuchumi za mataifa tajiri, matamshi ya wakati huu yanawakilisha shutuma kali dhidi ya baadhi ya washirika muhimu wa kibiashara.

Amesema kushindwa kwa Ulaya katika kutatua mzozo wake wa madeni kunakwamisha mataifa mengine duniani, sio tu kutokana na kupungua kwa biashara, lakini pia kunasababisha wasi wasi mkubwa katika masoko ya dunia.

Bwana Gordhan amesema hali hiyo inasababisha kuyumba kwa sarafu za nchi za Afrika kila siku, na kwamba viongozi wa ulaya hawataki kusikiliza nchi zingine.

Amewakosoa kuwa hawana uwezo wa kisiasa wa kusimamia nchi zao kwa upande mmoja, na kuhakikisha hawaangamizi uchumi wa dunia kwa upande mwingine.

Bwana Gordhan ameseme mzozo wa madeni barani Ulaya unazamisha nchi zote, na kutishia kusababisha hali kuwa mbaya zaidi katika muda wa miaka kumi ijayo.

Matamshi yake yameungwa mkono na Waziri wa Fedha wa Nigeria Ngozi Okonjo-Iweala, ambaye amesema mataifa tajiri yanaweza kujifunza kutoka nchi zinazoendelea kuhusu namna ya kudhibiti madeni na kuongeza ukuaji.