Rwanda kumenyana na Sudan nusu fainali

Kombe la Cecafa
Image caption Kombe la Cecafa

Rwanda itacheza dhidi ya Sudan katika nusu fainali ya Kombe la Cecafa Senior challenge kwa nchi za Afrika mashariki na kati.

Timu zote mbili zilifuzu kufuatia ushindi katika robo fainali siku ya Jumatatu.

Sudan waliwaondoa Burundi kwa kuwafunga mabao 2-0, ilhali Rwanda ilifuzu baada ya kuishinda Zanzibar mabao 2-1.

Amir Abdelnabi aliifungia Sudan katika kipindi cha kwanza, na bao la pili likafungwa na Musa Mohamed katika kipindi cha pili.

Rwanda ilifanikiwa kuibandua Zanzibar kufuatia bao la ushindi lililofungwa na Meddie Kagere dakika mbili kabla ya mechi kumalizika.

Amavubi walikuwa wameshafunga bao la kutangulia katika dakika ya 39 kupitia Jean Baptiste Mugiraneza, lakini muda mfupi baadaye Abdulrahman Mohammed akaisawazishia Zanzibar.

Robo fainali mbili zinachezwa Jumanne, huku Uganda ikichuana na Zimbabwe, nao wenyeji Tanzania bara wakipambana na Malawi.

Washindi kwenye robo fainali hizo ndio watakaokutana katika nusu fainali ya pili.

Nusu fainali kati ya Rwanda na Sudan itachezwa siku ya Alhamisi.