Kura rasmi za urais DRC kucheleweshwa

Makarani wa uchaguzi DRC

Tume ya Uchaguzi katika Jamuhuri Ya Kidemokrasia ya Congo imechelewesha kutangaza matokeo rasmi ya kura za urais hadi Alhamisi kutokana na matatizo ya usafirishwaji wa nakala za kujumlishwa kura.

Matokeo ya mapema yameonyesha rais wa sasa Joseph Kabila akiwa mbele ya upinzani ambao umesema hautamtambua Kabila kama rais baada ya hiyo jana ambayo ilikuwa siku rasmi kisheria kuwa rais wa Congo.

Tume ya uchaguzi iliomba msaada wa helikopta za Umoja wa Mataifa kusafirisha karatasi za kujumlisha kura huku makarani wa kujumlisha kura za taifa mjini Kinshasa wakiwa mbioni kumaliza hesabu yote kabla ya Jummanne. Hata hivyo masanduku ya kura ambazo hazikujumlishwa yalikuwa bado kufunguliwa hapo jana.

Afisa mmoja wa kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi amesema upande wake hautamtambua rais Kabila baada ya kipindi chake kumalizika chini ya katiba ya taifa.Wakati huo huo polisi wa kuzima ghasia wamekabiliana na wafuasi wa bwana Tshisekedi mjini Kinshasa. Shughuli za kawaida zimekwamishwa na taharuki zilizoko katika maeneo mengi nchini humo.