Sheria mpya za kuokoa uchumi wa Ulaya

Sarafu ya Euro mashakani Haki miliki ya picha Reuters

Rais wa Baraza kuu la Ulaya Herman Van Rompuy, amependekeza kuwepo sheria kali za kiuchumi kwa nchi zinazotumia sarafu ya Euro.

Ufaransa na Ujerumani zimeridhia kuwepo na azimio jipya ili kulinda uchumi wa kanda inayotumia sarafu ya Euro.

Hatua hii imepata uungwaji mkono na waziri wa fedha wa Marekani Timothy Geitner huku Uingereza ikionekana kusitasita.

Hata kabla ya kongamano la bara Ulaya kufanyika baadaye wiki hii, tayari zimejitokeza dalili za tofauti za kisiasa. Ufaransa na Ujerumani zimesema kuafikiana sheria za kusimamia kanda inayotumia sarafu ya Euro.

Naye rais wa baraza kuu linalosimamia nchi wanachama wa muungano wa Ulaya amependekeza hatua kadhaa kwa viongozi wote wa muungano huo.

Baadhi ya mapendekezo yake ni sambamba na msimamo wa Ufaransa na Ujerumani, huku mengine yakiwa tofauti.Herman Van Rompuy anataka kuwepo sheria kali bila kubadilisha mkataba wa Jumuiya ya Ulaya.

Wadadisi wanasema pendekezo lake halina athari zozote kwa maongozi ya nchi wanachama. Hata hivyo Ufaransa na Ujerumani zina msimamo tofauti na zimetaka sheria mpya za kiuchumi.

Ikiwa pendekezo hili halitakubalika na nchi 27 wanachama wa EU, itakuwa nafasi ya kuweka mkataba mpya kando ya azimio lililounda muungano wa Ulaya. Mkata huu utasimamia nchi 17 zinazotumia sarafu ya Euro na pia utatumiwa kwa nchi nyingine inayonuia kujiunga na muungano wa Ulaya.

Mpango huu unaonekana kuitenga Uingereza. Waziri Mkuu David Cameron amekuwa akishinikiza kwamba sharti makubaliano yote yazingatie matakwa ya taifa lake. Hata hivyo mataifa yote yanataka mkataba wa sasa ujumuishe mataifa wanachama wa EU.

Wadadisi wanasema hatua za sasa ni kuokoa uchumi wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro badala ya kuimarisha umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Ulaya.