Al Shabaab kwenye Twitter

Haki miliki ya picha reuters
Image caption Wapiganaji wa kundi la Al Shabaab

Kufuatia mapigano makali ya miezi kadhaa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, na wanajeshi wa Kenya kuvamia kusini mwa taifa hilo, mapigano yameendelea kwa muda sasa katika eneo hilo.

Upande mmoja wa mapigano hayo ni kundi la wapiganaji wa Kiislamu wa al Shabaab,upande wa pili katika vita hivyo ni wanajeshi wa serikali ya mpito. Wanajeshi wa kulinda amani wa Muungano wa Afrika, wale wa Kenya pamoja na Ethiopia pia wako katika vita hivyo.

Vita hivi sasa vimeingia katika mfumo mpya wa mawasiliano kupitia mtandao wa kijamii wa facebook na Twitter.

Mwandishi wa BBC, Mary Harper, amepata mwaliko kutoka kwa kundi la al-Shabaab kufuatilia harakati zao. Kwanza mawasiliano yalikuwa kwa lugha ya kiarabu. Baadaye kundi hilo lilibadilisha na kuanza kutumia lugha ya Kiingereza ili wapate kufahamika zaidi, taarifa nyingi zikiwa propaganda ya kijeshi.

Mawasiliano ya kwanza yalizungumzia makabiliano ambayo baadaye yalibadilika na kuwa mapigano makali ya miezi kadhaa kati ya wapiganaji hao wa kiislamu na wanajeshi wa serikali ya mpito wakisaidiwa na muungano wa majeshi ya Muungano wa Afrika, Amisom.

Hatua hii ni ushahidi kuwa vita ambavyo zamani vilipiganwa kwa silaha vinabadilika na sasa propaganda ndio mbinu mpya inayotumika.