Uganda na Rwanda zatinga fainali

Uganda na Rwanda zimetinga fainali ya mwaka huu ya mashindano ya Cecafa Senior Challenge Cup hapo jana kufuatia ushindi wa mechi zao za nusu fainali.

Rwanda ilihimili vishindo vya Sudan na kushinda bao 2-1 katika mechi ya kwanza.

Mechi iliyofuata adhuhuri Uganda ilididimiza matumaini ya wa Tanzania wakati nchi hiyo ikisherehekea miaka 50 ya Uhuru kwa kuichabanga 3-1.

Uganda Cranes sasa itachuana na watani wao Rwanda katika fainali itakayofanyika jijini Daresalam siku ya jumamosi.

Hata hivyo ilikua Kili Stars iliyotanguliza bao mnamo dakika ya 17 Mrisho Ngasa alipotumia fursa ya pasi maridadi kutoka kwa Mwinyi Kazimoto.

Ngassa aliwapiga chenga mabeke wa Uganda kabla ya kumpita kipa Abby Dhaira kwa bao la kwanza.

Dakika tano baada ya bao hilo kipa wa Kilimanjaro stars, Juma Kaseja alishangaa mwenyewe kwa jinsi alivyoweza kuokoa shuti kali la Godfrey Walusimbi kutoka eneo la hatari.

Uganda Cranes ilirudisha bao hilo baada ya mapumziko kufuatia mpira wa kona uliotiwa kimyani na nahodha Andy Mwesigwa.

Kwa kipindi cha dakika zote 90 pande zote zikashindwa kupata bao la ushindi na hivyo kusababisha mechi kuingia mda wa ziada ambapo Emmanuel Okwi na Isack Sinde kuhitimisha kilichowapeleka Daresalam, ushindi.

Kocha wa Uganda Bobby Williamson aliiambia BBC kuwa ilibidi wabadili mfumo ili kupata ushindi huo. Kocha huyo akielezea mchuano wa jumamosi alisema anafahamu Rwanda ni Timu kali lakini atajiandaa vyema.

Rwanda iliishtua Sudan -ambayo ni nchi pekee kutoka kanda ya Afrika mashariki na kati itakayoshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani. Magoli ya Rwanda yalifungwa na Jean Claude Iranzi na Olivier Karekezi.