Wachache wapiga kura Ivory Coast

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Ouatarra apiga kura mjini Abidjan

Idadi ya wapiga kura waliojitokeza kwenye uchaguzi wa kwanza wa wabunge nchini Ivory Coast mwaka mmoja baada ya fujo,imekuwa ndogo sana.

Watu milioni tano walisajiliwa kupiga kura lakini chama cha Laurent Gbagbo, ambaye kukataa kwake kuondoka madarakani ndiyo kulichochea fujo,kimesusia uchaguzi huo.

Uchaguzi ulimalizika kwa amani, hata katika maeneo yanayomuunga mkono Gbagbo.

Rais Alassane Ouattara anasema uchaguzi huo ni hatua muhimu katika kurudisha demokrasia nchini Ivory Coast.

Vikosi vya Umoja wa Mataifa vilikuwa vinashika doria katika mji wa kibiashara, Abidjan.

Bwana Gbagbo yuko katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu akisubiri hatma ya mashtaka dhidi yake ya mateso dhidi ya binaadamu.

Chama cha Bwana Gbagbo, Ivorian Popular Front, kimeshtumu tume ya uchaguzi nchini humo kwa kumpendelea Rais wa sasa, Alassane Ouattara.

Pia kimedai kuwa jeshi limekuwa likitoa vitisho kwa wanachama wao wakati wa kampeni za uchaguzi.