Pakistan kutoza NATO ushuru

Maofisa wa Pakistan wanasema kua wanatafakari kutoza kodi na malipo kwa mamilioni ya dola za Marekani kwa kila mwaka kwa magari ya NATO yanayosafirisha mafuta na bidhaa za askari wa shirika hilo.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waziri mkuu Syed Razi Gilan

Ikumbukwe kua Pakistan ilifunga mpaka wake kwa vikosi vya NATO kufuatia shambulio la ndege za NATO ambapo askari wanne waliuawa.

Hadi leo raia wengi nchini Pakistan bado wana hasira kutokana na kitendo cha ndege za NATO karibu na mpaka wa nchi yao na Afghanistan, ambapo askari 24 waliuliwa. Tukio hilo limeleta mvutano baina ya Marekani na Pakistan na uhusiano huo kwa sasa umedorora mno.

Wengine wanauonelea uwamuzi wa Pakistan wa kufunga mpaka kwa Marekani na NATO punde baada ya shambulio kama ishara ya kulipiza kisasi. Kwa NATO njia ya barabara kupitia Pakistan ni sehemu muhimu ya kuvisaidia vikosi na operesheni zinazoendelea nchini Afghanistan.

Wanasema kua hadi sasa mazungumzo juu ya njia hio ni maneno tu yasiyo rasmi. Lakini wameongezea kua labda wakati umewadia kuanza mazungumzo rasmi ya makubaliano rasmi ambayo yatazingatia pia ushuru juu ya mafuta, uharibifu wa barabara kodi ya mapato kwa matumizi ya bandari na hifadhi.

Gharama hizo zinaweza kufikia hadi mamilioni mengi ya dola kwa kila mwaka, wamesema. Yote haya yanajitokeza wakati Pakistan ikiitisha mkutano wa siku mbili kujadili uhusiano wake na nchi za magharibi,hasa Marekani, kufuatia shambulio la NATO.

Mkutano huo utakaosimamiwa na Waziri wa mashauri ya kigeni wa Pakistan utahudhuriwa na hadi Mabalozi 15 wa ataifa ya magharibi.

Wakati hayo yakiendelea, maelfu ya magari ya kusafirishia mafuta na bidhaa nyingine yameachwa katika kusubiri katika maeneo mbalimbali ya Pakistan. Mengi yanaonekana kukabiliwa na hatari. Katika kipindi cha siku mbili zilizopita msafara ulishambuliwa huko Baluchistan, Pakistan ya kusini magharibi ka kushambuliwa kwa moto,risasi na makombora ya kurushwa.