Wananchi Misri waanza kupiga kura

mabango ya uchaguzi nchini Misri Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mabango ya uchaguzi nchini Misri

Raia wa Misri wanapiga kura kwenye awamu ya pili ya uchaguzi wa bunge jipya, ambao ni wa kwanza tangu kuondolewa madarakani kwa Rais Hosni Mubarak mwezi Februari.

Kwenye awamu ya kwanza ya uchaguzi mapema mwezi huu, vyama vya makundi ya Kiislamu vilishinda viti vingi, huku kile cha Muslim Brotherhood's Freedom and Justice kikipata asilimia 36.6 ya kura.

Inatarajiwa chama hicho kitadumisha ushindi huo wiki hii, wakati uchaguzi ukifanyika maeneo ya mashambani na yasiyopendelea mabadiliko.

Mchakato wa uchaguzi huo wa Misri ni mgumu na hautarajiwi kumalizika hadi mwezi ujao.

Lengo ni kuchagua bunge dogo ambalo litateua kamati itakayoandika rasimu ya katiba mpya ya utawala wa baada ya mapinduzi.

Uchaguzi umepangwa kufanyika katika kipindi cha miezi mitatu ili kuiwezesha idara ya mahakama kusimamia kwa uangalifu kila awamu ya uchaguzi huo.

Chini ya mfumo wa uchaguzi wa Misri, theluthi mbili ya wabunge 498 katika baraza la waakilishi watateuliwa kwa kuzingatia usawa wa uwakilishi, kwa kutumia orodha zilizoandaliwa na vyama na miungano.

Viti vitakavyosalia vitajazwa kupitia mfumo wa mshindi aliyeongoza, huku kila mgombea akitakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura, ili kuepuka marudio ya uchaguzi.

Awamu ya pili ya uchaguzi inafanyika katika majimbo tisa, mkiwemo baadhi ya maeneo ya nje ya mji mkuu Cairo, na maeneo ya mashambani ambayo kawaida yanakuwa ngome ya wanasiasa wanaozingatia uislamu.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa mbili asubuhi na upigaji kura unatarajiwa kuendelea kwa siku mbili.

Awamu ya tatu itafanyika mwezi Januari, nao uchaguzi wa urais utafanyika kati kati mwa mwaka 2012.

Rais Mubarak aling'atuka madarakani mwezi Februari kufuatia maandamano mjini Cairo na sehemu zingine za nchi, yaliyochukua muda wa majuma kadhaa.

Jeshi lilichukua uongozi wa nchi, lakini limekuwa likilaumiwa kwa kujaribu kuchelewesha mabadiliko ili kukabidhi khatamu kwa utawala wa kiraia.

Waandamanaji walirudi barabarani tena, na mwezi uliopita kulikuwa na makabiliano makali kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji walioghadhabishwa na kasi ndogo ya mabadiliko.