Marekani : uchaguzi DRC una 'dosari '

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kiongozi wa Upinzani Tshisekedi adai yeye ndiye aliyeshinda

Uchaguzi wa hivi karibuni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ulikuwa "na dosari nyingi ", Marekani imeonya wakati ikitoa wito wa mchakato huo kutahminiwa tena upya.

Matokeo rasmi yamempa Rais Joseph Kabila ushindi wa asilimia 49% dhidi ya asilimia 32% ya kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi.

Lakini matokeo hayo yamekosolewa na Jumuiya ya Ulaya,kituo cha Carter Center na waangalizi wengine wa uchaguzi.

Balozi wa Marekani nchini humo anasema kumekuwa na "dosari kadhaa".

"Marekani inaamini kuwa uendeshwaji wa uchaguzi huu ulikuwa na dosari," Balozi James Entwistle alisema katika taarifa kwa shirika la habari la Reuters.

"Uchaguzi haukuwa wazi na haukuzingatia mafanikio ya demokrasia yaliyoonekana katika chaguzi za nchi zingine barani Afrika," alisema.

Bwana Entwistle alisema Marekani na wafadhili wengine kutoka nchi za Magharibi wanatoa msaada wa kiufundi kwa Congo ili kuchunguza kwa makini dosari zilizotambuliwa na waangalizi wa uchaguzi, jambo ambalo tayari limeafikiwa na waziri mkuu wa nchi hiyo, alisema.