Iraq yajaribu kupatanisha Syria

Ujumbe wa serikali ya Iraq umekwenda Syria, kuisihi serikali iache kutumia nguvu nchini humo.

Haki miliki ya picha AFP

Ujumbe huo unaongozwa na Waziri wa Usalama wa Iraq, Falah al-Fayadh, na unasema kuwa unawasiliana na upinzani wa Syria pamoja na serikali.

Wairaqi wanajaribu kupatanisha ili kufanywe mazungumzo yatayofuata mapendekezo ya amani yaliyotolewa na Jumuia ya nchi za Kiarabu.

Mwandishi wa BBC anasema, Wairaqi wanafikiri wanaungwa mkono na Marekani katika juhudi hizo, na haikuelekea kuwa watafanya ziara hiyo bila angalau kuungwa mkono na Iran.

Ziara hiyo inafanywa wakati kundi kuu la upinzani la Syria - Syrian National Council -- linakutana Tunisia.

Linatarajiwa kujadili mkakati wake wa kujitayarisha kama serikali kivuli, tayari kuchukua madaraka Rais Assad akiondoka.