Saif-al-Islam Gaddafi ‘hajamwona wakili’

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Saif al-Islam mtoto wa Kanali Gaddafi hajaonana na wakili tangu akamatwe Libya

Saif al-Islam Gaddafi, mtoto wa Kanali Mummar Gaddafi hajamwona wakili tangu akamatwe, mtetezi wa haki za binadamu ameiambia BBC.

Hata hivyo, Saif al-Islam hana malalamiko ya kutendewa vibaya, kwa mujibu wa Fred Abrahams wa Human Rights Watch.

Bw Abrahams ametoa wito kwa mamlaka ya Libya kumpa fursa ya kuonana na wakili ‘haraka iwezekanavyo.’

Saif al-Islam alikamatwa mwezi uliopita wakati akijaribu kukimbia Libya.

Ni mtu anayetakiwa sana kutoka utawala uliopita.

Bw Abrahams alisema mamlaka ya Libya ilimruhusu kwa muda wa nusu saa kuwa na Saif al-Islam katika mji wa Zintan, ambako anashikiliwa.

Hali ya kiafya ya Saif al-Islam ilikuwa "nzuri" na laifanyiwa upasuaji wiki mbili zilizopita kutibu mkono wake uliojeruhiwa, Bw Abrahams alisema.

Waendesha mashtaka walisema Saif al-Islam atapata fursa ya kuonana na wakili mapema wakati anahamishiwa sehemu nyingine yenye ulinzi katika mji mkuu wa Tripoli, aliongeza.

Saif al-Islam alilalamika kwa Bw Abrahams kwa kile alichokiita ‘kutengwa’, akisema wakati maafisa wakimtembelea hajaruhusiwa kumwona mtu yeyote wa chaguo lake.

Bw Abrahams alisema amepata hisia kutoka kwenye mkutano wake na Saif al-Islam "hailewi vizuri kuwa sasa si mmoja wa watu wenye nguvu nchini mwake,"

Saif al-Islam anatakiwa na mahakama ya ICC kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mahakama ya ICC imekubali kwamba kesi yake iendeshwe ndani ya Libya kwa masharti yatakayowekwa na Baraza la Mpito la Taifa.

Waziri mkuu wa Libya Abdurrahim al-Keib ameahidi kuwa kesi ya Saif al-Islam itaendeshwa kwa haki.