Marekani yashutumu Syria kwa dhuluma

Marekani imesema hatua inapaswa kuchukuliwa dhidi ya Serikali ya Syria kwa kuwatesa waandamanaji.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Syria, Bashar al-Assad, akihutubia mkutano siku zilizopita.

Katika taarifa kali sana tangu maasi ya wananchi dhidi ya Serikali kuanza nchini Syria, Serikali ya Marekani imesema kuwa wanajeshi wa Syria wamekuwa wakiwaua na kuwatesa waandamanaji nchini humo.

Marekani pia ilitoa wito wa kutekelezwa kwa mpango wa amani wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu wa kurejesha amani nchini humo.

Mpango huo usipotekelezwa vikwazo vikali zaidi vya kijamii na kiuchumi vitachukuliwa dhidi ya Syria, Ikulu ya White house imenukuliwa ikisema katika taarifa yake.

Makundi ya upinzani yamesema kuwa zaidi ya watu 200 wameuawa katika muda wa siku mbili zilizopita.

Hii leo Jumuiya ya mataifa ya Kiarabu inatuma ujumbe wa kundi la wachunguzi kuingia nchini Syria ili kusisitiza kumalizika kwa vurugu.

Kwa upande wake Syria inasema kuwa inakabiliana na magenge ya magaidi yenye silaha, ambayo yanataka kuvuruga amani na utangamano nchini humo.

Syria ni taifa ambalo limekumbwa na maasi ya wananchi kuanzia mwezi wa tatu, wakati ambapo mataifa ya Kiarabu kama vile Tunisia, Libya na Misri yamekabiliwa na hali ambayo viongozi wake wametimuliwa mamlakani; ambapo mmoja wao ni Muammar Gaddafi wa Libya aliyeuawa na waasi waliompinga.