Kiongozi kijana wa ANC akata rufaa

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bw Julius Malema

Kiongozi wa vijana wa Afrika Kusini aliyesimamishwa Julius Malema amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa chama tawala wa kumfukuza.

Alisimamishwa na African National Congress (ANC) kwa miaka mitano kutokana na kuleta mgawanyiko ndani ya chama.

Mawakili wa Malema wanadai uamuzi huo haukufuata utaratibu halisi wa ANC na kutaka ubatilishwe.

Aliyewahi kuwa mshirika wa karibu wa rais Jacob Zuma, Bw Malema sasa anamshutumu kwa kuwapuuza Waafrika kusini walio maskini waliompigia kura kuingia madarakani mwaka 2009.

Rufaa ya Bw Malema mbele ya jopo la rufaa ya kinidhamu iko kwa kiwango kikubwa katika misingi ya madai kwamba kamati hiyo haikumpa fursa ya kujitetea ambayo ingeweza kumpunguzia hukumu mwishoni mwa mchakato wa nidhamu.

ANC ilimsimamisha mwezi Novemba 2011 baada ya kukutwa na hatia ya makosa matatu yanayomkabili- ikiwemo kuipotezea heshima chama kwa kutoa wito wa kutaka mabadiliko ya uongozi huko Botswana- jambo linaloingiliana na sera za chama na serikali.

Bw Malema, ambaye aliwahi kusema anaweza hata kuua kwa ajili ya rais Zuma yupo katika ushindani wa kutaka kumtoa kama mwenyekiti wa ANC na badala yake anataka naibu rais Kgalema Motlanthe achukue nafasi yake, amesema mwandishi wa BBC wa Johannesburg Milton Nkosi.

Kiongozi wa ANC moja kwa moja huwa mgombea wa chama- hivyo hukubalika zaidi- katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo mwaka 2014.