Maandamano yasitishwa Nigeria

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Maandamano Nigeria

Vyama vya wafanyakazi vya Nigeria vimesema vinasitisha kwa muda maandamano kwa siku mbili kuruhusu mazungumzo zaidi na serikali.

Tangazo hilo limetolewa siku ya tano ya maandamano baada ya kuondolewa ruzuku ya mafuta, zilizosababisha bei ya mafuta na nauli kupanda mara dufu.

Maelfu ya watu wanaandamana, huku watu kadhaa wakiwa wamefariki dunia kutokana na makabiliano na polisi.

Vyama hivyo vilisema mazungumzo yaliyofanyika siku ya Alhamis na Rais "yanaridhisha" na yataendelea siku ya Jumamosi.

Mashirika makuu ya vyama hivyo kwa pamoja yalitangaza kutokuwepo na maandamano mwishoni mwa juma na safari za ndege zitaanza upya, na kuwapa nafasi viongozi kusafiri kuelekea mji mkuu, Abuja kwa ajili ya mazungumzo.

Vyama vya wafanyakazi wa mafuta vilisema vitasitisha kuzalisha mafuta kwenye nchi hiyo inayouza mafuta mengi nje ya nchi barani Afrika, kuanzia siku ya Jumapili.

"Tunataka kuhakikisha kwamba Jumamosi na Jumapili- tunapumzika, " kiongozi wa Nigeria Labour Congress Abdulwahed Omar aliuambia mkusanyiko wa watu kwenye mji mkuu, Abuja.

"Lakini Jumatatu asubuhi, maandamano yatakuwa makubwa kuwahi kutokea," alisema, shirika la habari la AFP limeripoti.

Asilimia 80 ya pato la Nigeria linatokana na mafuta lakini baada ya miaka mingi ya rushwa na ubadhirifu, imeshindwa kuhimili kusafisha mafuta, ambayo inabidi kuuzwa ndani ya nchi.

Serikali imeahidi kutumia dola za kimarekani milioni nane inayotumia kila mwaka kwenye ruzuku hizo kuimarisha shule, huduma za afya na usambazaji wa umeme.

Lakini Wanigeria wengi maskini wanahofia itaishia mifukoni mwa maafisa, ambapo wanaona mafuta ya bei rahisi ni faida pekee wanayoipata kutoka kwenye utajiri wa mafuta wa nchi hiyo