Naibu Jaji Mkuu Kenya kuchunguzwa

Haki miliki ya picha online
Image caption Nancy Baraza, Naibu Jaji Mkuu Kenya katika uchunguzi kwa madai ya kumtishia mlinzi kwa bastola

Polisi nchini Kenya inafanya uchunguzi baada ya Naibu Jaji Mkuu nchini humo Nancy Baraza kudaiwa kumtishia mlinzi mmoja wa kike kwa bastola katika eneo moja la kibiashara mjini Nairobi.

Kiongozi huyo wa mahakama aliombwa afanyiwe ukaguzi wa kiusalama kabla ya kuingia dukani kwa nia ya kununua dawa.

Kamishina wa mkuu wa polisi nchini Kenya Mathew Iteere amethibitisha kuamrisha uchunguzi wa kisa hicho ambapo naibu jaji mkuu Nancy Baraza alimtishia mlinzi wa kike katika eneo moja kibiashara mjini Nairobi.

Mlinzi huyo kwa jina Rebecca Morara aliwaeleza polisi kwamba alikuwa akifanya ukaguzi wa kiusalama kwa wateja katika jengo la maduka ya kifahari maarufu mjini Nairobi la Village Market.

Mlinzi huyo aliongeza kuwa Naibu Jaji Mkuu alipita bila kukaguliwa hatua iliyomlazimu kumsihi afuate utaratibu uliowekwa.

Morara ameongeza 'Bi Baraza badala yake aliamua kurudi kwenye gari lake na baadaye akarejea huku akiwa ameshika bastola na kuanza kunitishia.' Morara alimjulisha mkuu wa kitengo cha ulinzi cha soko hilo ambaye alimshauri kuwasilisha taarifa kwa polisi.

Tukio hilo limepokelewa kwa hisia tofauti huku wengine wakishangaa kutokana na hadhi ya Naibu Jaji Mkuu na sifa zake za kutetea maadili mema na sheria kufuatwa.

Kwa mujibu wa Bi Baraza kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, hakumtisha mlinzi huyo kwa njia aina yeyote.

Naibu Jaji Mkuu hajazungumzia tukio hilo kwa undani kutokana na uchunguzi wa polisi unaoendelea.

Amekanusha kuwa na nia ya kumtisha au kumkejeli raia wa Kenya.

Ameongeza kuwa anaelewa hali ya usalama nchini na kwamba ni hatua ambazo binafsi amechukua kama mmoja wa maafisa wakuu serikalini.

Amewaomba Wakenya kusubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi ambao utabaini ukweli.

Katika miezi ya karibuni usalama umeimarishwa katika maeneo mengi nchini kufuatia tisho la mashambulizi ya kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab baada ya jeshi la Kenya kuingia Somalia kukabiliana na wapiganaji hao.

Wapiganaji hao wanatuhumiwa kuhusika na mashambulizi kadhaa ya gruneti ambapo raia na maafisa wa usalama waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Wasi wasi huu umefanya maeneo ya kibiashara yakiwemo majengo ya ibada kuweka utaratibu mkali kuwakagua watu wanaoingia maeneo hayo.