Mubarak anyongwe anadai Mshtaki mkuu

Mubarak Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mubarak akifikishwa mahakamani

Waendesha mashtaka katika kesi ya rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak wametaka apewe adhabu ya kifo.

Bw Mubarak anashtakiwa mjini Cairo kwa makosa ya kuamrisha mauaji ya waandamanaji, wakati wa ghasia zilizosababisha rais huyo kuondolewa madfarakani mwaka jana.

Waendesha mashtaka pia wanataka adhabu ya kifo itolewe kwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi Habib el-Adly na wakuu sita wa zamani wa usalama.

Zaidi ya waandamanaji 800 waliuawa katika siku 18 za maandamano kabla ya Bw Mubarak kuondolewa madarakani Februari 11.

"Hukumu yoyote ya haki lazima iwe ya kifo kwa washtakiwa hawa," amesema Mustafa Khater akikaririwa na shirika la habari la AFP.

"Kamwe hawezi, kama kiongozi wa nchi, kudai kuwa hakufahamu kinachoendelea," amesema mwendesha mashtaka mkuu Mustafa Suleiman akiiambia mahakama.

"Anahusika na lazima abebe majukumu ya kisheria na kisiasa kwa kilichotokea", ameongeza.

Kwa kutazama ukubwa wa mashtaka, kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kutaka adhabu ya kifo itolewe, lakini wananchi wengi wa Misri watashitushwa kwa kusikia madai hayo yakitolewa waziwazi kwa mara ya kwanza katika kesi hii, anasema mwandishi wa BBC mjini Cairo, Jon Leyne. Hata hivyo, iwapo Bw Mubarak atauawa au hata kukutwa na hatia ni swala tofauti, kwani upande wa mashtaka umelalamika ukosefu wa ushirikiano kutoka wizara ya mabo ya ndani katika kutoa ushahidi na kesi hiyo imedhoofika kutokana na shahidi mkuu kubadili ushahidi wake, amesema.

Upande wa mashtaka umesema umechukua ushahidi kutoka kwa watu 2,000, wakiwemo maafisa wa polisi ambao walijadili amri zilizotoka juu za kuwa na silaha na kuzitumia dhidi ya waandmanaji.

Baadhi ya watu waliokuwa na nguvu nchini MIsri wametoa ushahidi wao tangu kesi hiyo ilipoanza mwezi Agosti.