Ngumi zarushwa bungeni Somalia

Sharif hassan Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Sharif Hassan alipigiwa kura zenye utata kuondolewa

Serikali ya Somalia imeanzisha uchunguzi kufuatia ngumi kurushwa ndani ya bunge mjini Mogadishu kutokana na mzozo wa kuchaguliwa kwa spika mpya.

Ngumi zilirushwa, wabunge kurushiana viti, na wengine walitumia kalamu kuwachoma wenzao. Wabunge watatu walipelekwa hospitali kwa majeraha.

Hatimaye spika mpya alichaguliwa baadaye siku ya Jumatano, lakini rais amesema hautambui uchaguzi huo.

Serikali ya mpito ya Somalia inaungwa mkono kimataifa, lakini inakabiliwa na shutuma za mizozo ya kikoo.

al-Shabaab

Kwa msaada wa majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika, serikali hiyo kwa sasa inadhibiti mji wa Mogadishu, lakini kundi la al-Shabaab ambalo lina uhusiano la al-Qaeda, bado linadhibiti maeneo mengi ya kati na kusini mwa nchi hiyo.

Nchi hiyo imeghubikwa na vita kwa miaka ishirini na haijakuwa na serikali kamili ya kuchaguliwa tangu mwaka 1991.

Hii si mara ya kwanza katika wiki za hivi karibuni kwa mapigano kuzuka bungeni.

Mwandishi wa BBC Will Ross anasema mzozo wa hivi karibuni umekuwa mbaya zaidi kuliko mapigano yaliyowahi kutokea bungeni.

Kinyume cha sheria

Mapigano ya Jumatano jioni yalianzishwa na wafuasi wa Sharif Hassan Sheikh Aden, ambaye alipigiwa kura ya kuondolewa nafasi ya uspika kwa njia za utata mwezi uliopita.

Wafuasi wake hawakutaka uchaguzi wa spika mpya kufanyika. Rais Sharif Sheikh Ahmed anasisitiza kuwa Bw Aden bado ni spika na kwa hiyo bado haifahamiki kwa sasa nani ndio spika halisi.

Amesema uchaguzi wa Madobe Nunow haukuwa wa haki na kinyume cha sheria, kwa sababu mpango wa amani ambao uliunda serikali ya mpito haukuwapa wabunge nguvu ya kufanya uamuzi kama huo.

Baadhi ya wachambuzi wanasema rais anaogopa huenda na yeye akapigiwa kura ya kuondolewa madarakani.

Siku ya Alhamis asubuhi rais huyo aliongoza mkutano kuhusu sakata la wabunge, ambao kama mwenyekiti alieleza kuwa "hasara iliyopatikana katika vifaa vya bunge ni jambo la kusikitisha" imesema taarifa.

Kamati hiyo pia "imeomba radhi kwa wananchi wa Somalia kuhusiana na jambo hilo lisilo na msingi".

Mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilionya serikali kuacha mapigano ya ndani kwa ndani ama sivyo itapoteza misaada inayopewa na Umoja wa Mataifa.