Kijana auawa kwa imani za uchawi London

Mahakama Haki miliki ya picha skyscan
Image caption Kesi inasikilizwa mahakam kuu

Mahakama Kuu mjini London - Old Bailey - imesikiliza kesi ya jinsi kijana wa miaka kumi na tano alivyoteswa na kuuawa na dada yake akishirikiana na rafiki yake wa kiume kwa sababu waliamini kuwa kijana huyo alikuwa mchawi.

Kristy Bamu, kutoka Paris, alikutwa amekufa eneo la Newham, Mashariki mwa London, siku ya Krismasi mwaka 2010.

Kijana huyo alikutwa na majeruha 101 na alikufa kutokana na kupigwa kwa kipande cha bati na kuuawa, mahakama imeelezwa.

Ukatili

Dada yake Mgalie Bamu na mpenzi wake, Eric Bikubi, wote wakiwa wametokea nchini Congo na wote wakiwa na umri wa miaka 28, kutoka eneo la Newham, wamekana kuhusika na mauaji hayo.

Waendesha mashtaka wamewaelezea wazee wa baraza kuwa ni matendo ya uovu na ukatili.

Bw Bikubi alikiri kuua bila kukusudia kwa misingi ya uzembe, jambo lililokataliwa na upande wa mashtaka.

Kristy na ndugu zake walikuwa wakiwatembelea wapenzi hao siku ya Krismasi, lakini Bw Bikubi alimshutumu kijana huyo na ndugu zake wawili kwa uchawi.

Bafuni

Wote watatu walipigwa, na watoto wengine walilazimishwa kujihusisha kwenye shambulio hilo. Mwendesha mashtaka alisema, lakini Kristy ndio akawa amedhamiriwa hasa na Bw Bikubi.

Inasadikiwa kijana huyo alikuwa na maumivu makali baada ya siku kadhaa za kupigwa na silaha mbalimbali zikiwemo, fimbo, koleo, chuma, nyundo na patasi huku akilia 'bora afe'.

Mwendesha mashtaka Brian Altamna alisema, hatimaye Bikubi alimpeleka bafuni, na kumfungulia maji yatiririke.

Kristy alikuwa amejeruhiwa sana na mwenye uchovu wa kupambana na hata kunyanyua kichwa chake kipate maji.

Mateso

Ni pale tu Bw Bikubi alipogundua Kristy alikuwa hasogei ndipo alipoacha na kumtoa kwenye maji.

Mwendesha mashtaka aliongeza mpaka kufikia wakati huo alishachelewa.

Wadogo zake walilazimishwa kusema uongo kwa wazazi wao kuhusu kilichotokea walipopiga simu, wazee wa baraza walielezwa.

Mwendesha mashtaka Altman alisema baba wa watoto hao aliwapeleka watoto wao likizo na si kwenye chumba cha mateso.

Wachawi

Polisi walipowasili eneo hilo walimkuta Kristy na ndugu zake, Yves amabye ni kaka yake mwenye umri wa miaka 22, na dada yake Kelly mwenye umri wa miaka 20, na watoto wengine.

Bw Altman alisema, wote walikuwa wamesimama ukumbini, wakiwa na woga na wamerowa. Hakuna hata mmoja wao aliyekuwa akizungumza Kiingereza.

Kelly Bamu alisema Bw Bikubi na Bi Bamu walimshutumu Kristy, yeye mwenyewe na mtoto mwengine wa tatu kwa kuwa wachawi.

Watatu hao walipigwa na kunyimwa chakula, vinywaji na kulala, na hatimaye ili kuwafanya waache kuwatesa, walikiri kwamba wao ni wachawi, baraza la wazee waliambiwa.

Washtakiwa hao wametoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na wazee wa baraza waliambiwa kuwa uchawi unaojulikana kwa jina la kindoki unatumika sana kwenye makanisa ya Congo.

Kesi hiyo inaendelea.