Uchina yasema Marekani ni mchokozi

Gazeti la taifa la Uchina limechapisha makala yanayoishutumu Marekani kuwa "mchokozi", katika mvutano unaozidi Mashariki mwa Asia.

Haki miliki ya picha AFP

Makala hayo yanafuatia sera mpya ya ulinzi iliyotangazwa na Marekani, ambayo inasema italenga eneo la Asia.

Katika taarifa ya ukurasa wa mbele, gazeti la People's Daily, la chama tawala cha Kikoministi cha Uchina, Adimeri Yang Yi anasema ni wazi kuwa mkakati mpya wa ulinzi wa Marekani, unazilenga Uchina na Iran.

Adimeri huyo anailaumu Marekani kwa matokeo ya miaka miwili iliyopita, ambayo amesema yanatishia usalama wa Asia.

Hakueleza matokeo yenyewe.

Aliongeza kusema kuwa ni wazi kuona nani ni mchokozi katika usalama wa eneo hilo.

Taarifa hiyo siyo ya serikali, lakini lazima ilipitishwa na serikali kuwekwa ukurasa wa mbele namna hivo.

Sera mpya ya Marekani iliyotangazwa juma hili, inasema mipango ya ulinzi ya Marekani sasa italenga Asia.

Kuna uwezekano wa kushirikiana na Uchina, lakini ilisema haijulikani wazi nini msimamo wa kijeshi wa Uchina.

Kwa hivo Marekani itahakikisha kuwa ina nguvu kuonesha masilahi yake Asia, na itazidisha maingiliano na washirika wake katika eneo hilo.