Wageni waonywa watahadhari Kenya

Wizara ya Mashauri ya Nchi za Nje ya Uingereza imeonya wageni nchini Kenya, kwamba kuna tishio kubwa la mashambulio ya kigaidi.

Haki miliki ya picha 1

Wizara hiyo inasema inaamini kuwa magaidi wanaweza kuwa katika hatua za mwisho za mpango wa kufanya mashambulio, na kwamba wageni waepuke maofisi ya Kenya pamoja na maeneo ambako wageni na watalii kuhusanyika, kama mahoteli, maeneo ya maduka mengi na pwani.

Watalii kama milioni-moja walizuru kenya mwaka jana, asili-mia-10 zaidi kushinda mwaka uliotangulia.

Polisi wa Kenya wanaopambana na ugaidi hivi karibuni walimkamata raia mmoja wa Uingereza, na wanaamini kuwa wamegundua njama kubwa.

Piya wanawasaka raia wengine wawili wa Uingereza nchini Kenya ambao wanafikiriwa kuwa wana uhusiano na al-Shabaab.

Kikundi cha wapiganaji wa al-Shabaab cha Somalia kimeshafanya mashambulio kadha nchini Kenya, na wamewateka watalii mwambao wa nchi hiyo.