Iran ina kiwanda cha siri cha nyuklia

Kiwanda cha Nyuklia Haki miliki ya picha AFP
Image caption Marekani inasema Iran inafanya uchokozi

Iran imeanza kurutubisha madini ya Uranium katika kiwanda kilichoko chini ya ardhi kaskazini mwa nchi hiyo.

Shirika la kimataifa la kawi ya kitonoradi, limedhibitisha kuwa shughuli za kurutubisha madini hayo zinaendelea katika kiwanda hicho cha Fordo.

Wakuu wa serikali ya marekani mjini Washington wanasema tangazo hilo la Iran ni uchochezi.

Victoria Nuland, msemaji katika ofisi ya rais anasema kiwango hicho kikubwa cha kurutubisha madini ya uranium kimechochea zaidi hofu zao kuhusu madai kuwa mradi huo wa Iran wa nyuklia ni wa amani.

Anasema madini ya Uranium yakirutubishwa hadi kiwango cha asilimia 20, huwa sawa na silaha.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague, amesema hatua za Iran wakati ambapo jumuiya ya kimataifa imekuwa ikiisihi Tehran itoe maelezo kuhusu mradi huo ni za uchokozi.

Kwa muda wa miezi kadhaa sasa uhusiano kati ya Iran na nchi za magharibi umekuwa mbaya. Wiki iliopita marekani iliiwekea vikwazo benki kuu ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya ulitangaza kuzuia mauzo ya mafuta ya Iran.

Kufuatia hatua hizo, nayo Iran ilitishia kufunga mkondo wa bahari wa Hormuz ambapo zaidi ya asilimia 20 ya mafuta kote duniani hupitia.

Tishio hilo lilijibiwa mara moja na Waziri wa ulinzi wa marekani Leon Panetta ambaye alisema Marekani itachukua hatua kufungua mkondo huo ikiwa utafungwa.

Wakati huo huo, serikali ya Iran imemfungulia mashataka ya ujasusi raia mmoja wa Marekani mwenye asili ya nchi hiyo.

Utawala mjini Tehran unasema Amir Hekmati alikuwa anafanya kazi na shirika la kijasusi la marekani CIA, na alikuwa akifanya uchunguzi nchini humo.

Hata hivyo, familia ya mtu huyo inasema alikuwa nchini Iran kutembelea mababu zake. Marekani imesema mashataka hayo dhidi yake ni ya kusingiziwa.

Kwa kipindi cha mwaka mmoja watu kadhaa wanaoshukiwa kuwa majasusi wameuawa nchini Iran na hatma ya Hekmati itabaini uhusiano wa siku za usoni kati ya nchi hizo mbili.