Uchunguzi wa nani alimuua Habyarimana

Rwanda Haki miliki ya picha Sygma
Image caption Mauaji ya Kimbari yalianza baada ya ndege kudunguliwa

Wataalam wanaochunguza kudunguliwa kwa ndege ya aliyekuwa rais wa Rwanda mwaka 1994 Juvenal Habyarimana wanatarajiwa kusema shambulio hilo lilitoka wapi.

Wataalam hao - waliopewa jukumu na Ufaransa - wametembelea eneo la tukio kutazama jinsi bomu hilo lilivyorushwa.

Hii pia huenda ikaonesha nani hasa anahusika na shambulio hilo lililoanzisha mauaji ya kimbari.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na Ufaransa ulimtupia lawama rais wa sasa Paul Kagame, lakini serikali yake imesema Wahutu wenye itikadi kali ndio walimuua kiongozi wao.

Waasi

Ndege hiyo iliyodunguliwa Aprili 6 1994 - ambayo Bw Habyarimana na rais wa Burundi walikuwemo ndani - ilichochea kuanza kwa mauaji ya kimbari ambapo Watutsi 800,00 na Wahutu wenye msimamo wa kati waliuawa katika siku 100 tu.

Mauaji hayo yalisimama wakati kundi la waasi la Kitusti la RPF likiongozwa na Bw Kagame, lilipoteka mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Mwaka 2006, jaji mmoja nchini Ufaransa alimtuhumu Bw Kagame na washirika wake kwa kumuua Bw Habyarimana - tuhuma ambazo rais huyo amezitupilia mbali na jambo ambali lilisababisha kiongozi huyo kuvunja uhusiano na Ufaransa kwa miaka mitatu kuanzia 2006.

Msimamo wa kati

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mabaki ya ndege ya Habyarimana

Miaka mitano baadaye, mshirika wa zamani wa ngazi ya juu wa rais Theogene Rudasingwa - ambaye alikuwa katibu mkuu wa RPF na akiwa na cheo cha meja wakati wa mauaji ya kimbari - pia alimtuhumu Bw Kagame. Bw Rudasingwa alikosana na rais huyo na sasa anaishi uhamishoni nchini Marekani.

Bw Kagame anasisitiza kuwa Wahutu wenye msimamo mkali - ambao walimuona Bw Habyarimana ana msimamo wa kati - walidungua ndege na kutupia lawama RPF ili kupata kisingizio cha kuendesha mauaji ambayo tayari walikuwa wameyapanga.

Wakosoaji wa uchunguzi wa mwaka 2006 wanasema hawakufika katika eneo la tukio, au hata kuwahoji maafisa tisa wa ngazi ya juu wa RPF ambao walituhumiwa kuhusika.

Mfululizo wa matukio

Jaji Marc Trevidic wa Ufaransa anaongoza uchunguzi wa sasa, ambao ulianzishwa - na kupata msaada kamilifu kutoka kwa mamlaka za Rwanda - mwishoni mwa mwaka 2010 kwa sababu wafanyakazi wa Ufaransa pia walikufa katika shambulio hilo.

Wachunguzi hao wamewahoji watu sita wanaotuhumiwa katika ripoti ya mwaka 2006 na pia walifanya uchunguzi wa kisayansi. Wataalam wawili wa mabomu, wataalam wawili wa ajali za ndege, rubani mmoja, masoloveya wawili na mtaalam mmoja wa sauti wameunda upya eneo na mfululizo wa matukio.

Mwandishi wa BBC Christian Fraser mjini Paris anasema ripoti ya Trevidic itatoa baadhi ya majibu kwa maswali ya nani hasa alihusika na mauaji ya Habyarimana, lakini sio yote.

Rwanda imekuwa ikizongwa na mvutano wa kikabila, ambapo hali ilikuwa mbaya zaidi wakati wa utawala wa kikoloni chini ya Ubelgiji, wakati huo Watutsi mabao ni wachache walipata kazi nzuri na elimu kuliko Wahutu walio wengi.

Baada ya kupata uhuru, kufuatia ghasia za kikabila, maelfu ya Watutsi walikimbilia nchini Uganda, ambapo hatimaye walianzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1990.

Mwaka 1993 makubaliano ya amani yalitarajiwa kuanzisha serikali ya kugawana madaraka, lakini hatua hiyo haikusaidia kuondoa mvutano.