'Kagame hakudungua ndege' - Ripoti

Paul
Image caption Rais Kagame hakudungua ndege imesema ripoti

Ripoti ya uchunguzi imeonekana kumfutia tuhuma Rais wa Rwanda Paul Kagame za kuchochea mauaji wa kimbari ya mwaka 1994 kwa kudungua ndege ya rais wa wakati huo Juvenal Habyarimana.

Wataalam wa uchunguzi - waliopewa jukumu na Ufaransa - walitembelea eneo la tukio kutazama jinsi bomu lilivyorushwa na kudungua ndege hiyo.

Kudunguliwa kwa ndege hiyo ilikuwa moja ya vichocheo vilivyosababisha mauaji ya kimbari.

Uchunguzi wa awali wa Ufaransa ulimtupia lawama Bw Kagame na washirika wake, lakini ripoti ya sasa imesema Wahutu wenye itikadi kali ndio walimuua Habyarimana.

Serikali ya Rwanda imepokea kwa furaha majumuisho ya ripoti hiyo.

Ndege hiyo iliyodunguliwa Aprili 6 1994 - ambayo Bw Habyarimana na rais wa Burundi walikuwemo ndani - ilichochea kuanza kwa mauaji ya kimbari ambapo Watutsi 800,00 na Wahutu wenye msimamo wa kati waliuawa katika siku 100 tu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Watutsi 800,000 waliuawa

Mauaji hayo yalisimama wakati kundi la waasi la Kitusti la RPF likiongozwa na Bw Kagame, lilipoteka mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Waandishi wa habari waliofuatilia sakata hilo wamesema mahakama siku ya Jumanne ilifikia uamuzi kwamba bomu lilirushwa kutoka umbali wa takriban kilomita moja, na kuiudungua ndege hiyo iliyokuwa ikijiandaa kutua.

Kwa wakati huo, eneo hilo lilikuwa likishikiliwa na jeshi la Rwanda, kikosi maalum cha rais.

Tuhuma

Wataalam wamesema ingekuwa vigumu sana kwa wanajeshi wanaomtii Bw Kagame kuwepo katika eneo hilo na kuweza kuidungua ndege hiyo.

Wamesema ingekuwa rahisi zaidi kwa wanajeshi wa Habyarimana au wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa katika eneo hilo, kurusha bomu hilo.

Mwaka 2006, jaji mmoja nchini Ufaransa alimtuhumu Bw Kagame na washirika wake kwa kumuua Bw Habyarimana - tuhuma ambazo rais huyo amezitupilia mbali na jambo ambali lilisababisha kiongozi huyo kuvunja uhusiano na Ufaransa kwa miaka mitatu kuanzia 2006.

Miaka mitano baadaye, mshirika wa zamani wa ngazi ya juu wa rais Theogene Rudasingwa - ambaye alikuwa katibu mkuu wa RPF na akiwa na cheo cha meja wakati wa mauaji ya kimbari - pia alimtuhumu Bw Kagame. Bw Rudasingwa alikosana na rais huyo na sasa anaishi uhamishoni nchini Marekani.

Bw Kagame amekuwa akisisitiza kuwa Wahutu wenye msimamo mkali - ambao walimuona Bw Habyarimana ana msimamo wa kati - walidungua ndege na kutupia lawama RPF ili kupata kisingizio cha kuendesha mauaji ambayo tayari walikuwa wameyapanga.

Wakosoaji wa uchunguzi wa mwaka 2006 wanasema hawakufika katika eneo la tukio, au hata kuwahoji maafisa tisa wa ngazi ya juu wa RPF ambao walituhumiwa kuhusika.

Mfululizo wa matukio

Jaji Marc Trevidic wa Ufaransa anaongoza uchunguzi wa sasa, ambao ulianzishwa - na kupata msaada kamilifu kutoka kwa mamlaka za Rwanda - mwishoni mwa mwaka 2010 kwa sababu wafanyakazi wa Ufaransa pia walikufa katika shambulio hilo.

Wachunguzi hao wamewahoji watu sita wanaotuhumiwa katika ripoti ya mwaka 2006 na pia walifanya uchunguzi wa kisayansi. Wataalam wawili wa mabomu, wataalam wawili wa ajali za ndege, rubani mmoja, masoloveya wawili na mtaalam mmoja wa sauti wameunda upya eneo na mfululizo wa matukio.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mke wa Habyarima anataka mnunuaji wa bomu atafutwe

Kufuatia ripoti hiyo, jaji Trevedic ama anaweza kuifuta kesi hiyo au kuendelea na uchunguzi, ambao huenda ukamalizika kwa kesi ya mahakamani.

"Uamuzi wa leo unathuibitisha msimamo wa siku nyingi wa Rwanda kuhusiana na matukio ya Aprili 1994," amesema waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo, katika taarifa.

Wakili wa familia ya Habyarimana amesema hawajafurahishwa na majumuisho ya ripoti hiyo - akihoji uhakika wa wataalam hao - na bado pia wanataka mtu akutwe na hatia.

"Haijalishi mahala shambulio lilipofanywa," mtoto wa kuime wa Habyarimana Jean-Luc ameiambia BBC idhaa ya Maziwa Makuu.

"Muhimu ni nani aliyefyatua bomu hilo," amesema.

Mjane wa Habyarimana, Agathe, ameiambia BBC kuwa anataka wachunguzi wa Ufaransa watafute ni nani alinunua bomu hilo la Urusi ambalo lililipua ndege - kwa sababu hiyo itasaidia kutambua nani hasa anahusika.

Rwanda imekuwa ikizongwa na mvutano wa kikabila, ambapo hali ilikuwa mbaya zaidi wakati wa utawala wa kikoloni chini ya Ubelgiji, wakati huo Watutsi mabao ni wachache walipata kazi nzuri na elimu kuliko Wahutu walio wengi.

Baada ya kupata uhuru, kufuatia ghasia za kikabila, maelfu ya Watutsi walikimbilia nchini Uganda, ambapo hatimaye walianzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1990.

Mwaka 1993 makubaliano ya amani yalitarajiwa kuanzisha serikali ya kugawana madaraka, lakini hatua hiyo haikusaidia kuondoa mvutano.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii