WHO: Utoaji mimba usio salama waongezeka

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandamanaji wakipinga utoaji mimba Marekani, utafiti unaonyesha hari zaidi kwa wanawake kiafya

Kuongezeka kwa utoaji mimba duniani kunahatarisha afya za wanawake, watafiti wanasema.

Utafiti uliofanywa na shirika la Afya duniani-WHO unonyesha kuwa kiwango cha utoaji mimba duniani kimebakia kuwa asilimia 28 kwa kila wanawake 1,000

Hata hiyvo uwiano wa mimba zinazotolewa bila utaalamu kimepanda kutoka 44% mwaka 1995 hadi 49% mwaka 2008.

Jarida la Lancet, ambalo limetoa ripoti hiyo lilisema ‘takwimu hizo zinasikitisha sana’.

Utoaji mimba usio salama unachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya uzazi duniani, unafanyika nje ya taratibu za hospitali, kliniki na upasuaji, au bila kuwa na wataalamu wa kitabibu wenye sifa.

Wanawake wako katika hatari zaidi ya kupata maambukizo au kupoteza damu nyingi katika harakati hizo.

'Vifo vya uzazi'

Katika nchi zinazoendelea hasa zile zenye sheria kali za utoaji mimba, utoaji mwingi unaofanyika si salama huku 97% zinatolewa kwa njia hiyo Afrika.

Kwa kulinganisha, 95% ya utoaji mimba Latin Amerika zilitajwa kuwa si salama, ikishuka kwa 40% Asia, 15% Oceania na 9% Ulaya.

Kuziweka pamoja takwimu hizo ni jukumu gumu katika nchi ambazo sheria zake zinazuia. Wanasayansi walitumia taarifa za utafiti, takwimu rasmi na rekodi za hospitali.

Wameamua kuwa wakati kiwango cha utoaji mimba kinashuka tangu mwaka 1995, kiwango hicho sasa kimebakia palepale na kwa ujumla kuongezeka kwa idadi ya watu duniani kunamaanisha kuwa kulikuwa na mimba milioni 2.2 zaidi zilizotolewa mwaka 2008 ikilinganishwa na mwaka 2003.

Katika nchi zilizoendelea kiwango cha mimba zilizoishia kutolewa kilishuka kutoka 36% mwaka 1995 hadi 26% mwaka 2008.

Nchi zenye sheria zinazozuia utoaji mimba hazikuwa na kiwango chochote kilichoshuka na katika baadhi ya maeneo idadi imeongezeka.

Profesa Beverly Winikoff,kutoka Gynuity, taasisi ya New York inayohamasisha utoaji mimba salama aliandika katika jarida hilo la Lancet: "Utoaji mimba usio salama ni moja kati ya sababu kuu tano zinazochangia vifo vya uzazi na kusababisha kifo kimoja katika kila vifo vya uzazi saba au nane mwaka 2008.’

"Hata hivyo, utoaji mimba unapofanyika kwa taratibu za kitabibu na uangalizi, hatari ya kifo inapungua na karibu mara 14 chini zaidi ya wakati wa uzazi.

"Taarifa hizo zinaendelea kuthibitisha kile kinachofahamika kwa miongo mingi kuwa wanawake wanaotaka kutoa mimba wasizozitaka watafuta utoaji huo kwa gharama yoyote hata kama ni kinyume cha sheria au inahatarisha maisha yao."

Dr Richard Horton, mhariri wa Lancet alisema: "Takwimu hizi za sasa zinasikitisha sana. Hatua iliyopigwa miaka ya 1990 sasa ni kinyume.

"Shutuma, unyanyapaa na kufanya utoaji mimba kuwa kosa la jinai ni ukatili na mbinu iliyoshindwa."

Kate Hawkins, kutoka kitengo cha Jinsia na Maendeleo katika Taasisi ya Maendeleo ilisema: "Iwapo ni halali au si halali wanawake watatafuta pa kutoa mimba na watatoa.

"Utafiti huu unaonyesha kuwa mwaka 2008, 86% ya utoaji mimba ulitokea katika nchi zinazoendelea na karibu nusu ya hizo duniani kote hazikuwa salama’.

"Wanawake wanaendelea kufa katika idadi kubwa kwa sababu ya utoaji mimba usio salama, ni kashfa na kwamba sekta ya maendeleo inatakiwa kuthaminiwa."

Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza iligharamia kwa sehemu utafiti huo na Waziri wake ambaye ni mbunge Andrew Mitchell alisema ‘ni janga’ ambalo idadi ya mimba zinazotolewa ‘mitaani’ inazidi kuongezeka.

"Wanawake wawe na uwezo wao kuamua iwapo wanataka, lini na wanataka watoto wangapi, lakini hili si halisi kwani hawana fursa ya mpango wa uzazi.

"Katika miaka minne ijayo, misaada ya Uingereza itawapa wanawake milioni 10 fursa ya kinga za kisasa ambazo zitazuia mamilioni ya mimba zisizotarajiwa."