Libya ilikuwa na silaha za kemikali

Haki miliki ya picha AP
Image caption Serikali ya Gaddafi ilikuwa na silaha za kemikali

Kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi alikuwa na hazina ya silaha za kemikali, chombo kinachosimamia utekelezaji wa sheria inayopiga marufuku silaha kama hizo kimesema.

Taasisi ya Kuzuia silaha za Kemikali (OPCW) ilisema wakaguzi wake walitembelea Libya wiki hii.

Miongoni mwa silaha za kemikali walizozikuta zilikuwa ni pamoja na virutubisho vya sumu ya mvuke (sulphur mustard agent) inayoweza kuunguza vikali.

Viongozi wapya wa Libya waliuambia ujumbe wa wakaguzi hao kuhusu kuwepo kwa hazina hiyo mwaka jana baada ya kumuondoa Gaddafi madarakani.

"Wakaguzi hao wamethibitisha kuwepo kwa silaha hizo za kemilaki, ambayo zinahusisha ‘sulphur mustard agent’ ambayo haijatatengenzwa tayari kuwa silaha ya kutumiwa," OPCW ilisema.

"Wakati huo huo, wakati wa ombi la mamlaka ya Libya, wakaguzi hao walikagua silaha, hasa mabomu ya mizinga ambayo waliyatambua kuwa ni silaha za kemikali na hivyo kutolewa taarifa."

‘Lengo la kimataifa’

Wakaguzi walisema silaha zote hizo zilizotangazwa zimehifadhiwa katika ghala ya Ruwagha, Kusini-Mashariki mwa nchi.

Ilisema serikali ya Gaddafi ilifanikiwa kuangamiza 54% ya silaha za kemikali ilizotangaza kuwa nazo kabla ya operesheni kuahirishwa mwezi Februari 2011 wakati ghala hiyo ilipoacha kufanya kazi.

Taasisi hiyo ya OPCW ilisema Libya sasa imepewa mpaka mwezi April 29 2012 kuwasilisha mpango kamili na tarehe ambayo kuteketezwa kwa malighafi ya silaha hizo kutakapokamilika.

Kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa kuangamiza silaha zote za kemilaki duniani uliosainiwa na Libya, hazina hizo zilitakiwa kuwa zimeangamizwa ifikapo tarehe 29 April 2012.

Hata hivyo, ucheleweshwaji wa hatua kufikia malengo hayo na baadhi ya watia saini mataifa mengine makubwa yenye hazina kama hizo ikiwemo Marekani na Urusi kuna maanisha kuwa makataa hayo yatafikiwa

Marekani imeridhia kuwa itachukua mpaka 2021 kukamilisha kuteketeza 10% ya silaha zake za kemikali.

Urusi bado iko nyuma zaidi ikiwa tayari imeshaharibu 48% ya hazina yake kubwa ya silaha za maangamizi za kemikali, OPCW ilisema.